Katika Sala ya Ijumaa Hyderabad, India

Rais Rouhani ataka Waislamu duniani waungane mbele ya maadui wengine wa Uislamu

Rais Rouhani ataka Waislamu duniani waungane mbele ya maadui wengine wa Uislamu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu kote duniani, mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel na maadui wengine wa Uislamu na Waislamu.

Rais Rouhani ametoa sisitizo hilo hii leo baada ya kuhudhuria Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Makka mjini Hyderabad, makao makuu ya mkoa wa Telangana kusini mwa India, ambapo pia amewataka Waislamu kote duniani kuiunga mkono kadhia ya Palestina.

Huku akishiria namna Mtume Muhammad SAW alivyokuwa akisisitiza mara kwa mara kuhusu umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu pasina kujali tofauti zao za kimadhehebu, Rais wa Iran amewataka Waislamu kukumbuka kila mara kuuombea umoja wao.

Amesema, "Iwapo jamii moja ya Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu inakabiliwa na changamoto fulani, basi ni kutokana na Waislamu kupuuza au kutofanyia kazi mafundisho halisi ya dini yao."

Kadhalika kwa mara nyingine tena Rais wa Iran amekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuitambua Quds Tukufu kuwa eti mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, chokochoko ambayo imelaaniwa vikali kote duniani.

Aidha Rais Hassan Rouhani amelaani kitendo cha Washington cha kupiga marukufu raia na wakimbizi kutoka nchi sita zenye iddadi kubwa ya Waislamu kuingia nchini Marekani na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa chuki za maadui dhidi ya Waislamu.

Rais wa Iran aliwasili nchini India jana Alkhamisi kwa ziara rasmi ya kikazi ya siku tatu, kufuatia mualiko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Narendra Modi.

Rais wa Iran ambaye ameandamana na Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hii, Alhamisi alikutana na viongozi wa Kiislamu mjini Hyderabad, ambapo alitahadharisha kuhusu njama za Wamagharibi za kujaribu kupanda mbegu za uhasama miongoni mwa Waislamu, kwa kuunda makundi ya kigaidi na wakufurishaji.
...............
300


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji
We are All Zakzaky