Umoja wa mataifa wataka mauaji ya Gaza yachunguzwe

Umoja wa mataifa wataka mauaji ya Gaza yachunguzwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kuwepo uchunguzi huru na wenye uwazi kuhusu mauaji ya waandamanaji 16 wa Kipalestina, waliouawa na wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kuwepo uchunguzi huru na wenye uwazi kuhusu mauaji ya waandamanaji 16 wa Kipalestina, waliouawa na wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza Ijumaa ya jana 30.03.2018.

Usiku wa Ijumaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura mjini New York, kufuatia ombi la Kuwait, lakini hakuna tangazo la pamoja lililoafikiwa kuhusu ghasia zilizojitokeza Ukanda wa Gaza. Makabiliano haya kati ya jeshi la Israel na Wapalestina ndio mabaya zaidi kutokea tangu vita vya mwaka 2014.

''Kuna wasiwasi kwamba hali hii inaweza kuzorota zaidi mnamo siku chache zijazo'', amesema Taye-Brook Zerihoun, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa umoja huo unataka pande husika zijizuie. Msemaji huyo vile vile amesema Umoja wa Mataifa uko tayari  kuzipa msukumo mpya juhudi za mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina.

Ufaransa pia imeonya kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa mzozo mpya katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kimabavu na Israel.

Mamia ya wapalestina wajeruhiwa

Wizara ya afya katika Ukanda wa Gaza imesema kwamba pamoja na watu 16 waliouawa, wengine 1,400 walikuwa wamejeruhiwa, wakiwemo 750 wenye majeraha ya risasi za moto.

Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel pamoja na Uingereza, zimesema zimesikitika kwamba kikao hicho kimefanyika wakati mbaya, sambamba na siku kuu muhimu ya dini ya Kiyahudi, hali iliyoufanya ujumbe wa Israel katika Umoja wa Mataifa usihudhurie kikao hicho.

Ni kwa sababu hiyo kwamba mabalozi wa nchi muhimu katika Baraza la Umoja wa Mataifa waliwakilishwa na wasaidizi wao, na hakuna tangazo lililoafikiwa katika kikao hicho.

Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour amesema amesikitishwa kwamba hakuna tangazo lililotolewa kulaani, ''mauaji yenye chuki dhidi ya waandamanaji wa amani'', wala wito wowote wa kuwalinda raia wa Kipalestina.

Israel yasema Wapalestina wanaeneza chuki

Israel, kupitia ujumbe wa maandishi uliotumwa na ubalozi wake katika Umoja wa Mataifa, imewashutumu wapalestina kutumia muda ambapo Wayahudi kote duniani wanasherehekea siku muhimu ya Pasaka, ''kueneza uongo dhidi ya Israel''.

Wanajeshi wa Israel wamewafyatulia risasi waandamanaji wa kipalestina waliosogelea mpaka wake ambao umejengewa ukuta imara, na kwa kutumia vifaru walivishambulia vituo vitatu vya chama cha Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Wapalestina wameishutumu Israel kutumia nguvu za ziada katika kuyakandamiza maandamano. Kwa upande wake Israel imeyataja maandamano hayo kama njama ya chama cha Hamas kutaka kufanya mashambulizi ndani ya Israel.

Hayo yanajiri huku wengi wakihisi kuzuka kwa vita vikali kati ya waisrael na wapalestina vita ambavyo vinasadikiwa kuwa na madhara makubwa kwa pande zoe mbili.

Mwisho wa habari / 291

 


Taarifa zinazohusiana

Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji
We are All Zakzaky