Marekani kufungua kurasa mpya ya mahusiano na Urusi

Marekani kufungua kurasa mpya ya mahusiano na Urusi

Marekani inajaribu kuiomba Urusi kuishawishi Iran itoe majeshi yake nchini Syria, kwani serikali ya Israel imekosa usingizi kabisa kutokana na uwepo wa majeshi ya Iran karibu na mipaka ya Israel.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Rais wa Marekani Donald Trump baada ya kukutana katika mkutano wake wa kilele na mwenzake wa Urusi nchini Finnland amesema dunia inatamani kuona uhusiano mwema wa Urusi na Marekani

Mkutano wa kilele kati ya rais Donald Trump wa Marekani na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin umemalizika huko Helsinki. Mkutano huo uliofunguliwa Jumatatu mchana ulikuwa unafuatiliwa na viongozi wa dunia na hasa barani Ulaya. Trump alifungua mkutano huo kwa kusema kwamba ulimwengu unataka kuiona Urusi na Marekani zikiwa katika uhusiano mzuri.

Rais  Donald Trump ameutaja  mkutano wake wa ana kwa ana na rais wa Urusi Vladmir Putin kama mwanzo mzuri. Hiyo ni kauli fupi aliyoitowa rais huyo wa Marekani mbele ya waandishi habari katika meza iliyokuwa imezungukwa na maafisa wa ngazi za juu mwanzoni mwa mkutano wa mchana ulioanza baada ya rais huyo kukutana na Putin katika kikao cha faragha kilichochukua muda wa masaa mawili wakiwa pamoja na wakalimani wao.

Miongoni mwa maafisa wa Marekani wa ngazi za juu waliojiunga na rais wao katika chakula cha mchana baada ya mkutano huo wa Faragha ni waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo,balozi wa Marekani nchini Urusi Jon Huntsman na wasaidizi wengine wa ngazi za juu. baada ya hapo Trump na Putin watazungumza mbele na waandishi habari katika mkutano wa pamoja muda wowote kutoka sasa.

Lakini Kabla ya mkutano wao wa  faragha viongozi hao wawili  walizungumza mbele ya waandishi habari wakiwa nje ya kasri la rais wa Finnland, Trump alianza moja kwa moja  kumpongeza rais Putin kwa maandalizi mazuri ya michuano ya soka ya Kombe la dunia yaliyomalizika jana Jumapili. Trump baadae akatangaza orodha ya masuali mengi atakayojadiliana na rais Putin  ingawa suala la kuhusu Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani mwaka 2016  hakuligusa hata kidogo.

''Muhimu kabisa ni kwamba tuna mengi mazuri yakuzungumza pamoja.Mambo yakuzungumzia ni kuanzia biashara,masuala ya kijeshi,makombora,Nyuklia mpaka suala la China. China tutaigusia kidogo kwasababu ni mshirika rais Xi ni mshirika wetu wa pamoja.''

Na  alipoulizwa na waandishi habari ikiwa atalizungumzia suala la Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani 2016 katika mkutano wa faragha na Putin hakujibu chochote.

Rais huyo wa Marekani pia akasema kwamba Marekani na Urusi hazijawahi kuwa katika masikilizano mazuri katika kipindi cha miaka kadhaa lakini anafikiri wataishia kuwa kwenye uhusiano mzuri kabisa na hicho ni kitu ambacho anafikiri ulimwengu unataka kukiona.

Upande wake rais Vladmir Putin amesema kwamba amekuwa akiwasiliana kwa simu na Trump pamoja na kukutana katika matukio ya kimataifa lakini umewadia wakati sasa wa kuwa na majadiliano ya kina kuhusu matatizo mbali mbali ya kimataifa na masuala tete. Wakati huohuo yamefanyika pia maandamano mjini Helsinki ya kupinga sera za Marais hao wawili wa Marekani na Urusi.

Marekani inajaribu kuiomba Urusi kuishawishi Iran itoe majeshi yake nchini Syria, kwani serikali ya Israel imekosa usingizi kabisa kutokana na uwepo wa majeshi ya Iran karibu na mipaka ya Israel.

Mwisho wa habari / 291

 


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

We are All Zakzaky