Rais wa Uturuki amtuhumu mwandishi wa habari kwa Ujasusi

Rais wa Uturuki amtuhumu mwandishi wa habari kwa Ujasusi

Rais Erdogan ameilaumu Ujerumani kwa kuunga mkono vitendo vya ugaidi. Mkutano mwingine wa waziri wa biashara wa Uturuki Nihat Zeybecki uliopangiwa kufanyika Jumapili katika mji wa Magahribi wa Frechen wazuiwa.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Rais Erdogan ameilaumu Ujerumani kwa kuunga mkono vitendo vya ugaidi.  Mkutano mwingine wa waziri wa biashara wa Uturuki Nihat Zeybecki uliopangiwa kufanyika Jumapili katika mji wa Magahribi wa Frechen wazuiwa.

Huku mvutano huo ukiendelea kupamba moto baina ya Uturuki na Ujerumani. Uturuki imemfungulia mashtaka mwandishi huyo wa habari wa Ujerumani yanayohusiana na kuendeleza propaganda kukiunga mkono chama cha kigaidi. Mwandishi Deniz Yucel anashtakiwa pia kwa kuunga mkono vuguvugu linaloendelezwa na kiongozi wa kidini Sheikh Fethullah Gulen aliye uhamishoni nchini Marekani. Gulen anatuhumiwa na rais Erdogan kuhusika na jaribio la mapinduzi la mwezi Julai mwaka jana lililoshindikana. 

Rais Erdogan na wizara ya mambo ya nje ya Uturuki wamekasirishwa na maamuzi yaliyopitishwa ya kufuta mikutano katika miji kadhaa nchini Ujerumani iliyopangwa kuhutubiwa na mawaziri wa Uturuki. Mikutano hiyo ilikuwa ni sehemu ya kuwashawishi raia wa Uturuki wapatao milioni 1.5 wenye haki ya kupiga kura miongoni mwa Waturuki milioni 3 wanaoishi nchini Ujerumani. 

Katika chaguzi za hivi karibuni asilimia 60 ya Waturuki wanaoishi Ujerumani walikipigia kura chama cha Erdogan cha AKP.  Lengo la kura hiyo ya maoni  itakayofanyika mwezi April ni kumuongezea mamlaka rais wa Uturuki. Rais Erdogan ametilia mkazo jambo hilo tangu mwezi Julai mwaka jana mara tu baada ya kushindikana kwa jaribio la kutaka kumpindua.

Erdogan amezilaumu nchi za Ulaya Magharibi kwa kushindwa kulaani kwa nguvu jaribio hilo la mapinduzi na badala yake amesema nchi hizo zimekuwa mstari wa mbele kumkosoa kwa kuendesha kamatakamata ya waandishi wa habari, wanasheria na wasomi miongoni mwa watu kutoka matabaka mbalimbali.  Hata hivyo Ujerumani imeyapuuza madai ya rais wa Uturuki

Katika mazungumzo kwa njia ya simu waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavosoglu na mwenziwe wa Ujerumani Sigmar Gabriel wamekubaliana kukutana hapa Ujerumani wiki ijayo tarehe 8 mwezi huu wa Machi kujadili mvutano uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Awali waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas aliomba kukutana na mwenziwe wa Uturuki Bekir Bozdag lakini waziri huyo alikataa. Maas amemwandikia barua kali waziri Bozdag baada ya waziri huyo kukataa kukutana naye.  Ujerumani ina wasiwasi juu ya mvutano huu unaoongezeka ikihofia Uturuki kubadili nia yake kutokana na kuukubali mpango wa kuwazuia mamilioni ya wakimbizi kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya ikiwa ni pamoja na Ujerumani.

Wakati huo huo serikali ya Uholanzi imesema  mipango ya serikali ya Uturuki ya kufanya mikutano katika mji wa Rotterdam sio sahihi.  Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alitarajiwa kuhutubia kwenye mkutano huo wiki ijayo nchini humo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa mara nyingine ameishutumu Uturuki kwa kuendelea kumzuia mwandishi habari wa Ujerumani Deniz Yucel.  Merkel amesema Ujerumani itaendelea kuunga mkono uhuru wa vyombo vya habari.  Kansela Merkel amesisitiza kwamba serikali ya Ujerumani haijiingizi katika maamuzi yanayopitishwa na serikali za majimbo.

Wakati huo huo wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani inaitaka Uturuki ijiepushe na hatua za kuuchochea zaidi mvutano huo.

Mwisho wa habari/ 291

 


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji
پیام امام خامنه ای به مسلمانان جهان به مناسبت حج 2016
We are All Zakzaky