Trump afanya juhudi kutatua mgogoro wa Qatar

Trump afanya juhudi kutatua mgogoro wa Qatar

Wakati mzozo wa kidiplomasia ukiendelea kati ya Qatar na mataifa mengine ya Kiarabu, Qatar inasema sasa Rais Donald Trump wa Marekani anachukuwa jitihada za kuukwamua mkwamo huo ulioshuhudia taifa hilo dogo likitengwa.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Wakati mzozo wa kidiplomasia ukiendelea kati ya Qatar na mataifa mengine ya Kiarabu, Qatar inasema sasa Rais Donald Trump wa Marekani anachukuwa jitihada za kuukwamua mkwamo huo ulioshuhudia taifa hilo dogo likitengwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani, amewaambia waandishi wa habari mjini Paris, Ufaransa, kwamba Trump, ambaye awali alikuwa amechukuwa msimamo mkali na mbaya dhidi ya Qatar, sasa anaongeza jitihada za kuona mgogoro huo unamalizika haraka.

"Msimamo wa Trump umeendelea kuwa hivyo hadi sasa na tumeshuhudia hamu kubwa akielezea haja ya kuutatua mgogoro huu. Rais Trump ameeleza wazi kwamba asingelipendelea kuona ugomvi baina ya marafiki. Tunakabiliwa na kitisho kinachofanana na lazina tulishughulikie hili haraka iwezakavyo," alisema waziri huyo.

Hakukuwa na kauli ya moja kwa moja kutoka Ikulu ya Marekani, White House, kuhusiana na maelezo hayo ya waziri wa nje wa Qatar, lakini inafahamika kuwa mwenyewe Trump aliwahi kusema mnamo mwezi Juni mwaka huu kuwa alishiriki kwenye kupanga hatua za kuiadhibu Qatar zilizochukuliwa na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, na Misri.

Ukiondoa Misri, mataifa mengine yote matatu yaliyoiwekea vikwazo Qatar ni wanachama wenziwe wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Mataifa ya Ghuba (GCC) na kwa pamoja wameshirikiana kampeni nyingi za kieneo na kimataifa.

Mataifa hayo yanasema serikali ya Qatar inamuunga mkono adui wao mkubwa kwenye eneo hilo, Iran, na pia makundi ya siasa kali, madai ambayo Qatar inayapinga.

"GCC wameigawa Qatar kwa Iran kama zawadi"

Kwa pamoja, mataifa hayo yamevunja mahusiano yote ya kidiplomasia, kisiasa na kibiashara na Qatar, hali ambayo imewaacha maelfu ya raia wakiwa wametengana na biashara kadhaa kufa. Vikwazo vilivyowekwa na mataifa hayo vinajumuisha usafiri wa ardhini, angani na baharini. 

Hata hivyo, Sheikh Mohammed al Thani amewaambia waandishi wa habari kuwa hali ya uchumi wa nchi yake ni nzuri, akionya kuwa hatua za mataifa hayo dhidi ya Qatar zinalifanya taifa hilo lenye utajiri wa gesi kuelekea zaidi kwa serikali ya Iran.

"Walikuwa wakiituhumu Qatar kwamba inajikaribisha na Iran, na sasa kwa hatua zao dhidi ya Qatar, wanaisukuma zaidi kuelekea Iran. Na wanaipa Iran, au taifa lolote kubwa kwenye eneo hilo, Qatar kama zawadi," waziri huyo aliwaambia waandishi wa habari.

Kuhusu Syria, waziri wa huyo wa mambo ya nje amesema nchi yake haijawahi kubadilisha msimamo wake. Qatar na Saudi Arabia zinawaunga mkono wanaotaka kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assadi, licha ya tafauti baina yao.

"Baada ya miezi minane, baada ya kuufanya mgogoro wa Syria kuwa wa kijeshi, hapo ndipo Qatar ilipoamua kuchukuwa upande. Tuliamua kusimama na watu," alisema Sheikh Mohammed, akiongeza kwamba kususiwa na mataifa mengine ya Ghuba hakuufanyi mtazamo wao kubadilika, kwani huko kutamaanisha "kuidharau misingi ambayo Qatar inaiamini."

Mwisho wa habari / 291

 

 

 


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji
We are All Zakzaky