Uingereza yapinga ushiriki wa Urusi katika kuchunguza shambulio la Sumu

Uingereza yapinga ushiriki wa Urusi katika kuchunguza shambulio la Sumu

Uingereza imelipinga pendekezo la kushirikiana na Urusi katika kufanya uchunguzi wa pamoja kuhusu kadhia ya mjini Salisbury ambapo jasusi wa zamani na binti yake walitiliwa sumu.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Uingereza imelipinga pendekezo la kushirikiana na Urusi katika kufanya uchunguzi wa pamoja kuhusu kadhia ya mjini Salisbury ambapo jasusi wa zamani na binti yake walitiliwa sumu.

Uingereza imepinga uwezekano wowote wa kuanzisha uchunguzi wa pamoja na Urusi kuhusu kutiliwa sumu kwa jasusi ndumilakuwili wa Urusi Skripal na binti yake katika mji wa Salisbury nchini Uingereza. Mkasa huo ulitokea mwezi uliopita.

Mjumbe wa Uingereza kwenye shirika la kupiga marufuku silaha za sumu OPCW ameliambia  baraza la utendaji la shirika hilo kwamba hakuna haja katika sheria za taasisi hiyo ya kumlazimisha  alietendewa uhalifu kushirikiana na mhalifu ili kufanya uchunguzi wa pamoja. Kaimu mjumbe huyo John Foggo amesema kufanya hivyo kutakuwa kinyume cha maadili.

Urusi imetoa wito wa kufanyika leo kikao maalumu cha baraza la utendaji la shirika hilo la kupiga marufuku silaha za sumu na imetaka kuwezeshwa kupata taarifa juu ya shambulio la sumu  lililofanyika katika mji wa Salisbury kusini mwa Uingereza tarahe 4 mwezi uliopita. Imeomba kikao hicho maalumu cha mjini The Hague kifanyike mwezi mmoja baada ya jasusi Skripal na binti yake Yulia kutiliwa sumu.Wajumbe wa  Uingereza wamesema kwenye kikao hicho maalumu kwamba maombi ya Urusi juu ya uchunguzi wa pamoja yana lengo la kupotosha na kutoa habari ambazo si sahihi ili viongozi wa Urusi waepuke  maswali wanayopaswakuyajibu. Wakati huo Urusi imesisitiza kushangazwa na hukumu iliyotolewa na mataifa ya Ulaya na Marekani ya kuwafukuza wanadiplomasia wa Urusi, kabla hata ya kuwa na uhakika kuwa Urusi imefanya shambulizi hilo.

Awali Gary Aitkenhead - Mtendaji Mkuu wa Maabara ya kiayansi ya nchini Uingereza ya Porton Down alielezea kuwa kwa upande wao kama wanasayansi waliweza kuitambua kemikali ya Novichok, na kutambua kwamba imo katika daraja la kijeshi ila hawakuweza kuthibitisha chanzo sahihi yaani wapi inapotoka sumu hiyo lakini wametoa taarifa za kisayansi kwa serikali ambayo imetumia pamoja na vyanzo vingine kufikia maamuzi iliyofikia

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi yake inaitarajia Uingereza na washirika kuheshimu sheria ya kimataifa ili kuumaliza mgogoro wa kidiplomasia. Putin ameyasema hayo katika ziara yake ya mjini Ankara, Uturuki amesema anaitumainia Uingereza na washirika wake kuacha vitendo vya kuharibu mahusiano ya kimataifa na kurudi katika mfumo wa sheria ya kimataifa.

Urusi na Uingereza zimelaumiana kwa undumakuwili na hadaa wakati ambapo wataalamu kwenye  shirikala kuzuia silaha za sumu wanajaribu kutoa habari za ufafanuzi juu ya shambulio la mjini  Salisbury .

Uingereza kwa kuungwa mkono na washirika wake wa barani Ulaya na Marekani wameitupia lawama Urusi kwa kufanya shambulio hilo.Lakini Urusi imekanusha vikali madai hayo. Urusi inaishikiniza Uingereza ili itoe ushahidi wa kuthibitisha kuwa ni Urusi iliyotenda uhalifu huo. Mkasa huo umesababisha uhusiano baina ya nchi za magharibi na Urusi ushuke hadi kiwango cha chini kabisa tangu kumalizika kwa vita baridi.

Kila upande umelipiza kisasi kwa kuwafukuza wanadiplomasia wa upande mwingine, Mkuu wa ujasusi nchini Urusi amedai kwamba shambulio hilo la sumu ni njama za Uingereza na Marekani. Mkuu huyo Sergei Naryshkin ambae ni mkurugenzi shirika la ujasusi wa nchi za nje amesema shambulio hilo ni uchokozi na kiburi uliofanywa na mashirika ya ujasusi  ya Uingereza na Marekani.

Akihutuba kwenye mkutano wa  kimataifa juu ya masuala ya usalama uliondaliwa na wizara ya ulinzi  ya Urusi, bwana Naryshkin amedai kuwa shambulio la Salisbury ni njama (mpya) za Marekani za  hivi karibuni zenye lengo la kuihujumu Urusi zinazofanana na mbinu za vita baridi.

Mwisho wa habari/ 291

 

 


Taarifa zinazohusiana

Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji
We are All Zakzaky