Muda unakaribia kwisha kabla ya viongozi wa Sudan Kusini kuunda serikali

  • Habari NO : 749086
  • Rejea : abna.ir
Brief

Jumuiya ya kimataifa imewapa muda viongozi wa Sudan Kusini Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar hadi kesho kufikia makubaliano na kuhakikisha Machar anarejea Juba ili kuundwe serikali ya mseto.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Jumuiya ya kimataifa imewapa muda viongozi wa Sudan Kusini Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar hadi kesho kufikia makubaliano na kuhakikisha Machar anarejea Juba ili kuundwe serikali ya mseto.

Mwenyekiti wa tume inayoungwa mkono na Jumuiya ya kimataifa ya uangalizi na tathimini ya pamoja JMEC Festus Mogae amesema iwapo watashindwa kukubaliana, basi makubaliano ya amani yatagonga ukuta.

Makubaliano hayo kati ya Kiir na Machar yalikusudia kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka miwili nchini Sudan Kusini na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine milioni mbili kuachwa bila ya makaazi.

Mustakabali wa taifa hilo changa zaidi duniani inategemea ni silaha kiasi gani na wanajeshi wangapi wa upande wa waasi wataruhusiwa kuandamana na kiongozi wa waasi Riek Machar.

Je Machar atarejea Juba kabla kesho?

Mogae amewaambia wanahabari kuwa watafanya mazungumzo zaidi leo na iwapo watashindwa kufikia makubaliano kuhusu hilo basi makubaliano hayo yatakuwa yamekwama kabisa.

Muda wa mwisho uliowekwa wa hapo kesho kwa viongozi wa Sudan Kusini kukubaliana, umependekezwa na wanachama wa JMEC ambao ni Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, China, Uingereza, Norway na Marekani.

Machar ambaye yuko katika taifa jirani la Ethiopia, anatarajiwa kufanya safari ya saa moja kwa ndege punde tu baada ya masharti ya pande zote mbili yatakapotimizwa na kuchukua wadhifa ambao alikuwa nao kabla ya vita wa Makamu wa Rais.

Kurejea kwa Machar mjini Juba na kuunda serikali ya Umoja wa kitaifa na Kiir kunaonekana kuwa nguzo muhimu ya kuhakikisha makubaliano ya amani yanatekelezwa.

Kiongozi huyo wa waasi alitarajiwa kuwasili Jumatatu wiki hii lakini akachelewesha safari hiyo kutokana na mvutano kuhusu ni wanajeshi wangapi na silaha kiasi gani anaweza kuwasili nazo.

Serikali imesema kiasi kikubwa cha wanajeshi na silaha hizo kutakiuka makubaliano hayo ya amani. Pendekezo la kimataifa lililokubaliwa na waasi ni kuwa walinzi wa Machar wanaruhusiwa kubeba bunduki za rashasha 20 na maguruneti yanayorushwa kwa roketi. Serikali inataka bunduki saba tu.

Kiasi cha wanajeshi na silaha chaleta mivutano

Alipoulizwa na wanahabari kitakachofuata iwapo muda wa mwisho hautaheshimiwa, Mogae amesema atalazimika kuwa ripoti viongozi wa Sudan Kusini katika Jumuiya ya ushirikiano wa kiamendeleo wa nchi za mashriki na pembe ya Afrika IGAD, Baraza la usalama la Umoja wa Afrika na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ili hatua muafaka zichukuliwe dhidi yao.

Waziri wa habari wa Sudan Kusini Miachel Makuei amesema pande zote mbili ziliombwa kwenda kutafakari hilo na kuja na mawazo ya namna bora zaidi ya kufikia suluhisho. Mjumbe wa waasi katika meza ya mazungumzo Tabna Deng Gai amesema wanakubali mapendekezo ya jumuiya ya kimataifa.

Kikosi cha wanajeshi 1,370 wa waasi kimewasili katika mji mkuu huku jeshi la serikali likisema lina wanajeshi 3,420 mjini Juba. Wanajeshi wengine wote wanapaswa kuwa takriban umbali wa kilomita 25 nje ya mji wa Juba.

Hapo jana, wapiganaji 100 wa waasi waliwasili Juba wakitokea Ethiopia na kuibua matumaini kuwa Machar huenda akawasili hivi karibuni.

Mwisho wa habari/ 291

 


Taarifa zinazohusiana

Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mahujaji
We are All Zakzaky