Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- , Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRNA), Hussein Jaberi Ansari, amesema kuwa vyombo vya habari kwa sasa ni miongoni mwa nguzo kuu za nguvu, ushawishi na hata usalama wa taifa kwa nchi mbalimbali duniani.
Jaberi Ansari alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake na Hujjatul-Islam Abdolreza Izadpanah, ambaye ni mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mkurugenzi anayesimamia Taasisi na Gazeti la Ettela'at Newspaper.
Katika mkutano huo, Jaberi Ansari alisisitiza kuwa sehemu muhimu ya mapambano yanayoendelea duniani leo haifanyiki tu katika nyanja za kijeshi au kisiasa, bali pia kupitia vyombo vya habari, operesheni za kisaikolojia, vita vya maarifa (cognitive warfare) na ushindani wa simulizi zinazolenga kuathiri mitazamo ya jamii na maamuzi ya kisiasa.
Alieleza kuwa katika mazingira ya sasa, uwezo wa kuwasilisha simulizi na kuathiri fikra za umma umekuwa sehemu muhimu ya nguvu za kimkakati za mataifa, jambo linalozifanya taasisi za habari kuwa na nafasi kubwa katika kulinda maslahi ya kitaifa.
Kwa upande mwingine, pande zote mbili katika mkutano huo zilisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa karibu kati ya IRNA na Taasisi ya Ettela'at, kwa lengo la kupanua wigo wa shughuli za habari, kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na kuimarisha mchango wa vyombo vya habari katika kukabiliana na changamoto za kisasa za kimawasiliano.
Washiriki wa mkutano huo walikubaliana kuwa kuongezeka kwa changamoto za vita vya habari na vita vya simulizi kunahitaji ushirikiano mkubwa zaidi kati ya taasisi za habari ili kuwasilisha ukweli na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu matukio ya ndani na ya kimataifa.
Your Comment