9 Agosti 2026 - 12:04
Araghchi: Iran itabaki thabiti kwenye ahadi ya mapambano; hatutasahau wala kusamehe uhalifu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema Iran haitaruhusu damu za watu waliouawa kwa dhulma zisahaulike au kupuuzwa, akisisitiza kuwa nchi hiyo itaendelea kushikamana na njia ya mapambano na upinzani dhidi ya dhulma na mifumo ya kibabe, licha ya shinikizo zote.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Iran itabaki thabiti kwenye ahadi yake ya kuendelea na njia ya mapambano na upinzani, huku akisisitiza kuwa taifa la Iran halitasahau wala kusamehe damu za watu waliomwagiwa kwa dhulma.

Araghchi ameyasema hayo leo Jumapili wakati wa hafla ya ufunguzi wa maonesho yenye mada ya “Muharram na A'shura katika Kioo cha Nyaraka za Wizara ya Mambo ya Nje”, ambapo alisema kuwa nyaraka zinazohusiana na Ashura zinaonesha kwa uwazi mapenzi ya ustaarabu wa Iran katika kukabiliana na mfumo wa hegemoni na nguvu za kikoloni.

Amesema diplomasia ya Iran, kama inavyoonekana katika nyaraka hizo, si diplomasia kavu, ngumu au inayojengwa juu ya maslahi ya muda mfupi, bali ni “diplomasia ya kibinadamu” inayoweka mwanadamu na maadili ya kibinadamu katika kitovu chake.

A'shura si tukio la kihistoria pekee, bali ni ustaarabu wa maisha
Katika hotuba yake, Araghchi amesema kuwa kumbukumbu ya Ashura imevuka mipaka ya kuwa tukio la kihistoria au kidini pekee na kuwa “shule ya maisha”, tamko la kudumu la kupigania haki na ukweli, pamoja na waraka wa msingi wa kupambana dhidi ya udhalimu, upotovu na ufisadi.

Kwa mujibu wa Araghchi, Mapinduzi ya Imam Hussein (as) yamekuwa lugha ya haki ya kimataifa na ujumbe wa kudumu wa kulinda heshima ya mwanadamu.

Amesema wananchi wa Iran wameifanya kwa karne nyingi shule ya Imam Hussein (as) kuwa sehemu muhimu ya maisha yao ya kiimani, kijamii na kitaifa, wakitumia mafundisho ya Ashura kama mwongozo wa kutafuta haki na kupinga mifumo ya kibabe katika medani ya kimataifa.

Nyaraka za Ashura zinaonesha nafasi ya Iran katika kueneza maadili ya kibinadamu
Waziri huyo amesema kuwa uchunguzi wa mamia ya nyaraka ambazo baadhi yake zinaoneshwa kwa mara ya kwanza unaonesha kwamba kulinda maeneo matakatifu na kuimarisha utamaduni wa Ashura kumekuwa sehemu isiyotenganishwa na dhamira ya kitaifa na utambulisho wa kidiplomasia wa Wairani.

Ametaja kuwa nyaraka hizo zinaeleza shughuli mbalimbali, kuanzia kuandaa na kuratibu shughuli za Ashura katika maeneo mbalimbali duniani, kusaidia Wairani wanaoishi nje ya nchi kuendesha majlisi za maombolezo, kurahisisha safari na huduma kwa mahujaji, hadi kushiriki katika ukarabati wa maeneo matakatifu na Haram za Maimamu (as).

Kwa mtazamo huo, amesema kuwa Ashura si urithi wa kidini pekee, bali pia ni urithi wa kimaadili, unaokumbusha dhulma na wakati huo huo kuwataka wanadamu kubeba jukumu la kuikabili.

Ujasiri hupimwa kwa utayari wa kujitoa kwa ajili ya haki”
Araghchi amesema kuwa ujumbe wa Imam Hussein (as) hauzuiliwi na mipaka ya kijiografia, bali ni lugha ya heshima ya mwanadamu inayokataa udhalilishaji, kutojali na udhalimu.

Amesema ujasiri wa kweli haupimwi kwa uwezo wa kutawala au kuvamia wengine, bali kwa utayari wa kujitoa kwa kiwango cha juu kabisa kwa ajili ya kutetea jambo la haki na misingi ya kibinadamu.

Kwa mujibu wake, urithi wa Imam Hussein (as) umefundisha kuwa kifo cha heshima ni bora kuliko maisha ya udhalilishaji, na kwamba uhuru unahitaji kujitoa na kujitolea.

Iran yasema itasimama imara mbele ya shinikizo
Akizungumzia hali ya sasa, Araghchi amesema Iran inakabiliwa na kile alichokiita wimbi la ukatili, udhalimu na vitisho, lakini akasisitiza kuwa taifa hilo halitaacha kulinda uhuru, heshima na mustakabali wake.

Amesema historia imeonesha kuwa mataifa yanapoacha kujitolea, kustahimili na kulinda uhuru wao, yanaweza kupoteza si ardhi pekee, bali pia utambulisho wao wa pamoja, matakwa ya kitaifa na uwezo wa kuamua mustakabali wao.

Kwa msingi huo, amesema Iran itaendelea kusimama imara kwenye ahadi yake ya upinzani na mapambano licha ya shinikizo zote.
“Hatutasahau, wala hatutasamehe”

Katika sehemu ya msimamo mkali zaidi wa hotuba yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa nchi hiyo haitaruhusu damu zilizomwagwa kwa dhulma kusahaulika au kupuuzwa.

“Hatutasahau wala hatutasamehe,” alisisitiza Araghchi, akieleza kuwa damu za waliouawa kwa dhulma zitaendelea kuimarisha njia ya kutafuta haki na kupambana dhidi ya udhalimu.

Ameongeza kuwa utamaduni wa kutafuta haki kwa ajili ya Imam Hussein (as) kwa zaidi ya miaka 1,400 haujabaki kuwa hisia za muda mfupi, bali umegeuka kuwa harakati ya kijamii na kisiasa inayobeba mwito wa haki na kupinga uhalifu na udhalimu.

Kwa kumalizia hotuba yake, Araghchi ameeleza matumaini kwamba maonesho ya “Muharram na Ashura katika Nyaraka za Wizara ya Mambo ya Nje” yatafungua njia ya kuelewa kwa undani zaidi uhusiano wa Wairani na Mapinduzi ya Ashura, pamoja na juhudi zao za kulinda maadili ya Kiislamu na heshima ya mwanadamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha