28 Septemba 2026 - 13:14
Dar-es-Salam: Madrasah ya Hazrat Fatima Zahra (sa) Yaadhimisha Maulid ya Mtume Muhammad (saww)

Madrasah ya Hazrat Fatima Zahra (sa), iliyopo Wazo–Kinondoni, Dar es Salaam, imeandaa hafla maalumu ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad Mustafa (saww), ikiwa na lengo la kuwakumbusha waumini na wanafunzi kuhusu mwenendo, maadili na mafundisho ya Mtume (saww).

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– DAR ES SALAAM: Madrasah ya Hazrat Fatima Zahra (sa), iliyopo eneo la Nyakasangwa–Wazo, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, imeandaa hafla maalumu ya kuadhimisha Maulid ya Mtume Muhammad Mustafa (saww).

Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 16 Septemba 2026, imekuwa sehemu ya shughuli za kielimu, kitamaduni na kidini zinazotekelezwa na taasisi na vituo vinavyohusishwa na Jamiat Al-Mustafa (s) Tanzania.

Madrasah ya Hazrat Fatima Zahra (sa) ni miongoni mwa vituo vya elimu ya Kiislamu vinavyohusishwa na Jamiat Al-Mustafa (s) Tanzania, vinavyoshughulika na ufundishaji wa elimu ya dini na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as), sambamba na kuendesha shughuli mbalimbali za kielimu, kitamaduni na kidini.

Hafla hiyo ilifanyika katika eneo la Madrasah na kuratibiwa chini ya usimamizi wa Ustadh Sheikh Maduwa Imran, huku ikihudhuriwa na wanafunzi, wazazi, walimu, walezi pamoja na waumini.

Katika hafla hiyo, Sheikh Abiyat alishiriki kama mzungumzaji na mgeni maalumu, ambapo alieleza kuhusu fadhila, tabia njema na sifa za kibinadamu za Mtume Muhammad Mustafa (saww).

Katika mawaidha yake, Sheikh Abiyat pia alieleza baadhi ya mafundisho ya kijamii na kimaadili ya Mtume Muhammad (saw), akisisitiza umuhimu wa kuyafahamu na kuyatekeleza katika maisha ya kila siku.

Akizungumzia nafasi ya Mtume Muhammad (saww) katika maisha ya mwanadamu, Sheikh Abiyat alieleza kuwa kutumwa kwa Mtume (saww) ni miongoni mwa neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani alitumwa kuwaongoza wanadamu na kuwafundisha njia sahihi ya kuishi katika maisha ya dunia kwa kuzingatia mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

Aidha, alisisitiza kuwa kumjua Mtume (saww) hakupaswi kuishia katika kutaja historia na fadhila zake, bali kunapaswa kuambatana na kujifunza mwenendo wake, kuhuisha mafundisho yake na kuyatekeleza katika maisha ya kila siku.

Mwisho wa hafla hiyo, msisitizo uliwekwa juu ya umuhimu wa kuifahamu Sira na Akhlaq ya Mtume Muhammad (saww), kuhuisha mafundisho yake na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha ya waumini.

Mafundisho hayo yanachangia katika kujenga jamii inayozingatia maadili mema, upendo, mshikamano, heshima na kuheshimiana, kwa kuufuata mfano wa Mtume Muhammad Mustafa (saww).

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha