Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt -ABNA- Ayatollah Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei, Amiri Mkuu wa Majeshi, katika ujumbe wake maalumu kwa kuadhimisha Wiki ya Jeshi la Polisi, ametoa shukrani zake kwa juhudi kubwa, kujitolea na ushujaa wa uongozi jasiri, makini na wenye busara wa FARJA (Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), pamoja na askari wake wazalendo na familia zao. Amelitaja FARJA kuwa miongoni mwa nguzo imara za usalama wa nchi, na kusisitiza kuwa kuimarishwa kwa pande zote kwa vikosi vinavyolinda usalama, hususan kupitia uboreshaji wa teknolojia na matumizi yenye malengo maalumu ya akili mnemba (AI), kuna nafasi muhimu katika kuboresha ubora na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Ifuatayo ni tafsiri ya ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Usalama ni miongoni mwa neema muhimu zaidi za Mwenyezi Mungu. Uimarishaji wa usalama huo katika maeneo mbalimbali ya Iran yetu pendwa, kuanzia miji mikubwa hadi vitengo vidogo kabisa vya makazi ya watu vijijini na mitaani; kuanzia maeneo magumu ya ulinzi wa mipaka yenye hali ngumu ya hewa na mandhari mbalimbali ya milima hadi baharini; na kuanzia tambarare na misitu hadi maeneo yaliyo katikati kabisa ya nchi, umetokana na ushujaa na ujasiri wa askari wa FARJA wanaojitolea na kufanya kazi kwa bidii. FARJA ni mojawapo ya nguzo imara za usalama wa nchi.
Usalama huu huwezesha kupatikana kwa hali mbalimbali za kijamii, maadili mema na utulivu wa umma katika jamii. Huduma hii yenye thamani kubwa, mbali na kuwa ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, pia inaungwa mkono na jamii kwa kiwango kikubwa.
Katika miaka ya hivi karibuni, nafasi muhimu ya FARJA katika ngazi mbalimbali, kuanzia ngazi za makamanda na makao makuu hadi vituo vya polisi na vituo vidogo vya ulinzi, katika kuhakikisha usalama, imezidi kudhihirika. Dalili za athari hii zilionekana wazi zaidi wakati wa vita vya pili na vya tatu vilivyolazimishwa dhidi ya Iran.
Msisitizo na juhudi za adui mhalifu wa Marekani na Uzayuni katika kushambulia ngazi mbalimbali za FARJA, kuanzia viongozi wa juu kabisa hadi askari wake wa ngazi za chini, pia zimeonesha wazi zaidi umuhimu wa taasisi hii.
Hata hivyo, juhudi hizi za kukata tamaa na mashambulizi hayo ya kikatili dhidi ya nguzo za utaratibu na usalama wa jamii, ambayo hayana mfano wake katika historia, hazikuwafanya askari jasiri wa FARJA kulegeza hata kidogo utekelezaji wa majukumu yao. Hata walipokuwa mitaani na ndani ya magari, waliendelea kutekeleza majukumu yale yale waliyokuwa wakiyafanya katika maeneo yao ya kazi na vituo vyao.
Kwa sababu hiyo, wananchi wa Iran, ambao licha ya kukabiliwa na dhuluma bado wana nguvu na msimamo thabiti, wanathamini juhudi na kazi zisizokoma za watumishi wanaolinda usalama wa nchi.
Kwa upande mwingine, askari wa FARJA, ambao kama vile Jeshi la Ulinzi na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) wanatokana na jamii yenyewe, wanaweza kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi hii yenye thamani kupitia mwenendo wao unaojenga uaminifu.
Wakati mwingine, juhudi na kujitolea kwa walinzi wa usalama huenda vikachukuliwa na baadhi ya watu kuwa ni mambo ya kawaida. Hali hii ya kutotambuliwa ipasavyo na kutokujulikana kwa mchango wao ndiyo inayoongeza malipo yao mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kuimarishwa kwa pande zote kwa vikosi vinavyolinda usalama, katika nyanja mbalimbali za rasilimali watu, vifaa na mifumo ya kiteknolojia, hususan kuboresha teknolojia, ikiwemo matumizi yenye malengo maalumu ya akili mnemba katika uchanganuzi wa data, kuna nafasi muhimu katika kuboresha ubora na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya FARJA.
Kwa kumwomba Mwenyezi Mungu awapandishe vyeo vya juu vya kiroho na kuwajalia radhi Zake mashahidi watukufu wa FARJA, na kwa kutoa shukrani kwa familia zote, wafanyakazi, wanajeshi wa kujitolea na askari jasiri na wenye moyo wa kizalendo, hususan kamanda jasiri, asiyechoka na mwenye busara wa FARJA, pamoja na juhudi zake kubwa; ninatumaini kwamba, kwa baraka za dua za Bwana wetu, Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), wataendelea kufanikiwa zaidi katika kuinua usalama, nguvu na heshima ya Iran ya Kiislamu.
Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei
Tarehe: 8 Oktoba 2026
Maoni yako