Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Katika ziara yake ya kitablighi, Maulana Sheikh Hemed Jalala, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C) amewavisha vilemba wanafunzi waliohitimu masomo yao ya dini baada ya kukamilisha kipindi cha miaka mitano ya masomo katika Hawzat al-Qaaim (atfs), iliyopo mjini Tanga, nchini Tanzania.
Shughuli hiyo iliambatana na hotuba fupi iliyotolewa na Maulana Sheikh Hemed Jalala, ambapo aliwapatia wahitimu nasaha na maelekezo muhimu kuhusu majukumu yanayowakabili baada ya kukamilisha masomo yao ya Hawza.

Katika nasaha zake, aliwahimiza wahitimu kutambua kuwa kuhitimu masomo ya dini si mwisho wa safari ya kutafuta elimu, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya kuitumikia dini ya Mwenyezi Mungu na kuisaidia jamii ya mwanadamu kupitia elimu waliyoipata.
Aidha, aliwasisitiza kuzingatia maadili mema, kuwa na mwenendo mwema, kuendeleza juhudi za kujifunza na kutumia elimu yao kwa hekima na busara katika kuwaongoza na kuwaelimisha watu katika jamii.
Shughuli hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha malezi ya wanazuoni na wahudumu wa dini wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao ya kielimu, kimalezi na kijamii kwa kuzingatia mafundisho ya Qur’ani Tukufu na Ahlul-Bayt (as).

Maoni yako