Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Yemen, katika taarifa yake, imetangaza kuwa shambulio la anga la Saudi Arabia dhidi ya msikiti mmoja katika eneo la Jashia, wilaya ya Hayfan, mkoani Taiz, ni uhalifu wa wazi.
Katika taarifa yake, tume hiyo imesema kuwa shambulio hilo la kihalifu dhidi ya moja ya nyumba za Mwenyezi Mungu limefichua sura halisi ya adui wa Kisaudi na Kizayuni, pamoja na kuweka wazi chuki yake ya muda mrefu dhidi ya maeneo matakatifu na alama za kidini za Umma wa Kiislamu.
Tume ya Haki za Binadamu ya Yemen imeeleza kuwa kulenga maeneo ya ibada na misikiti ni uhalifu wa wazi wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ambao umepigwa marufuku na dini zote zilizoteremshwa na sheria pamoja na mikataba ya kimataifa. Miongoni mwa sheria hizo ni Kifungu cha 53 cha Itifaki ya Ziada ya Kwanza ya Mikataba ya Geneva, Kifungu cha 27 cha Mkataba wa Nne wa Geneva na Kifungu cha 8 cha Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ambavyo vinakataza kulenga majengo yaliyotengwa kwa ajili ya ibada.
Tume hiyo imesema kuwa uhalifu huu umefichua na kubatilisha kabisa madai ya uongo na ya kupotosha ya utawala wa Saudi Arabia na vyombo vyake vya habari vinavyounga mkono sera zake, ambavyo vinadai kuwa Vikosi vya Wanajeshi vya Yemen vinalenga miji ya Makka na Madina.
Tume ya Haki za Binadamu ya Yemen imehoji: “Inawezekanaje mtu anayelinda maeneo matakatifu na kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu awe ndiye anayelenga Makka na Madina, wakati utawala wa Saudi Arabia wenyewe unalenga misikiti ya Mwenyezi Mungu nchini Yemen na kuwashambulia waumini kwa mabomu wakiwa katika sala?”
Utawala wa Saudi Arabia; mvamizi halisi wa maeneo matakatifu
Tume hiyo imesisitiza kuwa mtu anayelenga msikiti katika kijiji cha mbali cha Jashia, wilayani Hayfan, haoni tabu kutoa madai ya uongo kwamba Yemen inalenga Misikiti Mitakatifu Miwili ili kuhalalisha uvamizi wake.
Tume ya Haki za Binadamu ya Yemen imebainisha kuwa mvamizi halisi wa nyumba za Mwenyezi Mungu na maeneo matakatifu ni utawala wa Saudi Arabia na Kizayuni, huku watetezi wake wa kweli wakiwa ni wananchi wa Yemen na jeshi la nchi hiyo.
Tume hiyo imeutwisha utawala wa Saudi Arabia jukumu kamili la kisheria na jinai kuhusu uhalifu huo wa kutisha. Pia imesisitiza kuwa tukio hilo limeandikwa na kuwekwa katika kumbukumbu za uhalifu wa kimfumo, ambazo viongozi wa uvamizi watawajibishwa nazo katika mahakama za kimataifa.
Mwisho, Tume ya Haki za Binadamu ya Yemen imewaomba wanazuoni wa Umma wa Kiislamu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na jumuiya ya kimataifa kulaani uvamizi huu wa wazi dhidi ya nyumba za Mwenyezi Mungu na kufichua sera za viwango viwili za utawala wa Saudi Arabia, ambao kwa upande mmoja unadai kutetea maeneo matakatifu, lakini kwa upande mwingine unakuwa wa kwanza kukiuka heshima na utukufu wake.
Maoni yako