?>

Dola milioni 79 zinahitajika kunusuru meli iliyo hatarini kuzama Yemen

Dola milioni 79 zinahitajika kunusuru meli iliyo hatarini kuzama Yemen

Takribani dola milioni 38 zimechangishwa kati ya 79.6 zinazohitajika ili kunusuru meli ya kuhifadhi mafuta, FSO Safer iliyo hatarini kuzama na kuvujisha mafuta au kulipuka kando mwa pwani ya Yemen katika Bahari ya Sham.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo Duniani, UNDP nchini Yemen, limesema hayo kupitia mtandao wake wa Twitter Jumatano baada ya mkutano uliofanyika The Hague, Uholanzi kuchangisha fedha za kunusuru meli hiyo iliyoanza kuoza kwa kuweko baharini muda mrefu bila kukarabatiwa na bila kufanya shughuli zozote.

Safer ni meli ambayo ilitengenezwa mwaka 1976 kwa ajili ya kubeba na kusafirisha mafuta lakini muongo mmoja baadaye iligeuzwa na kufungwa mnyororo huku ikielea baharí kwa ajili ya  kuhifadhi mafuta.

Imefungwa mnyororo umbali wa maili za baharini 4.8 kutoka pwani ya jimbo la Hudaydah nchini Yemen ikiwa na mapipa milioni 1.14 ya mafuta ghafi.

Kazi ya kuzalisha, kushusha mafuta na kuikarabati ilisitishwa mwaka 2015 kutokana na vita nchini Yemen na sasa hali yake inazidi kuwa mbaya.

Tathmini inaonesha kuwa kwa sasa haiwezi tena kukarabatiwa na iko katika hatari ya mafuta kuanza kuvuja baharini au meli kulipuka.

Wataalamu wanasema Yemen haina uwezo wa kukabili madhara yatakayotokana na kuvuja au kulipuka kwa meli hiyo.

Gharama ya usafishaji iwapo mafuta yatavuja baharini ni dola bilioni 20 huku fedha zinazosakwa kutekeleza mpango wa kuinusuru ikiwa ni dola milioni 79.6.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema mpango wa Umoja wa Mataifa unaweza kuepusha janga kwa Safer kabla halijatokea.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*