?>

DRC yatangaza 'hali ya mzingiro' katika mikoa ya mashariki

DRC yatangaza 'hali ya mzingiro' katika mikoa ya mashariki

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza 'hali ya mzingiro' katika mikoa miwili ya mashariki mwa nchi inayoshuhudia mapigano na umwagaji damu kwa miezi kadhaa sasa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hayo yalitangazwa jana jioni na Patrick Muyaya, Msemaji wa Serikali ya DRC kwa niaba ya Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo na kueleza kuwa, mikoa hiyo ya mashariki inayoshuhudia ghasia tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa ni Ituri na Kivu Kaskazini.

Amesema lengo la tangazo hilo ni kutaka kukomeshwa haraka iwezekanavyo hali ya mchafukoge na ukosefu wa usalama katika mikoa hiyo. Msemaji wa Serikali ya Kongo DR amesema mapigano hayo hupelekea kuuawa kila uchao raia wasio na hatia katika mikoa hiyo.

Hata hivyo hajabainisha hatua zitakazochukuliwa na serikali na vyombo vya usalama katika mikoa hiyo baada ya kutolewa tangazo la 'hali ya mzingiro.'

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, watu zaidi ya 300 wameuawa katika mashambulio ya makundi yanayobeba silaha na katika mapigano ya kikabila katika mikoa hiyo ya mashariki mwa nchi tokea Januari mwaka huu hadi sasa.

Siku ya Alkhamisi, Rais Tshisekedi alitangaza kuwa, serikali yake inaandaa mikakati kabambe ya kukabiliana na utovu wa usalama katika eneo la mashariki mwa nchi.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*