?>

Hali ya hatari yatangazwa Ujerumani kutokana na COVID-19

Hali ya hatari yatangazwa Ujerumani kutokana na COVID-19

Wizara ya Afya Ujerumani imetangaza kuibuka wimbi jipya la maambukizi ya COVID-19 na hivyo kupelekea hali ya hatari kutangazwa katika nchi hiyo ya Ulaya Magharibi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Akizungumza na waandishi habari Ijumaa mjini Berlina, Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema wimbi jipya la visa COVID-19 au corona linalopiga kote Ujerumani limeitumbukiza nchi katika hali ya hatari, akiongeza kuwa hali sasa ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa wiki moja iliyopita.

Ijumaa Ujerumani ilirekodi maambukizi mapya 52,970 siku moja baada ya kurepoti kesi zingine 65,000 ambapo idadi hiyo ni ya juu zaidi tokea janga la corona lianze.

Wakuu wa serikali ya shirikisho na wa serikali za majimbo, wamekubaliana kuhusu hatua kadhaa mpya za kudhibiti wimbi jipya la janga la COVID-19.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuhimiza haja ya utoaji chanjo kwa wafanyakazi wote hospitalini na kwenye vituo vyote vya kuwauguza wagonjwa.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema nchi inakumbwa na hali tete na wakati umewadia wa kuchukua hatua.

Nayo nchi jirani ya Austria imekuwa nchi ya kwanza Magharibi mwa Ulaya kutangaza tena hatua za kufunga shughuli zote za kawaida katika msimu huu wa mapukutiko ili kupambana na wimbi jipya la maambikizi ya COVID-19.

Kansela wa wa nchi hiyo Alexander Schallenberg amesema hatua ya kufungwa shughuli za nchi kwa siku 10, na 20 ikizidi sana, akiongeza kuwa itakuwa lazima kwa kila raia kuchanjwa kuanzia Februari Mosi.

Aidha wiki hii Austria imekuwa nchi ya kwanza duniani kuwazuia kutoka nje watu ambao wamekataa chanjo ya COVID-19. Hata hivyo uamuzi huo umeibua maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Vienna.

Shirika la Afya Duniani lilitangaza kuwa bara Ulaya kwa mara nyingine ni kitovu cha maambukizi ya COVID-19 huku idadi ya wanaofariki barani humo ikiongezeka kwa kasi wiki iliyopita.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema wiki iliyopita, karibu watu milioni mbili waliambukizwa COVID-19 hii ikiwa ni idadi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa kwa wiki tokea mwanzo wa janga la COVID-19.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*