?>

Hamas: Uamuzi wa kuakhirisha uchaguzi ni mapinduzi dhidi ya maamuzi ya Wapalestina

Hamas: Uamuzi wa kuakhirisha uchaguzi ni mapinduzi dhidi ya maamuzi ya Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepinga vikali uamuzi uliochukuliwa na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas wa kuakhirisha uchaguzi mkuu na imeutambua uamuzi huo kuwa ni mapinduzi dhidi ya mchakato wa kuwepo ushirikiano baina ya harakati ya makundi ya kupigania uhuru wa Palestina na maafikiano ya kitaifa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na harakati ya Hamas imeeleza kusikitishwa sana na uamuzi huo wa Mahmoud Abbas na kusema maamuzi ya taifa zina la Palestina hayapaswi kutekwa na ajenda ya kundi moja la kisiasa.

Hamas imembebesha Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina lawama zote za uamuzi wa kucheleweshwa uchaguzi mkuu. Taarifa ya Hamas imesema kuwa, Wapalestina wanaoishi katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds (Jerusalem) wanaweza kulazimisha matakwa yao kwa utawala vamizi wa Israel na kufanya uchaguzi katika eneo hilo la Palestina.

Taarifa hiyo ya Hamas imetolewa baada ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, kutangaza rasmi habari ya kuakhirishwa uchaguzi mkuu wa Palestina, suala ambalo limeibua hasira na ghasia kubwa.

Katika taarifa ya jana Ijumaa, Abbas alisema uchaguzi huo umeakhirishwa kutokana na kuwa kwa sasa hauwezi kufanyika katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na Israel na ambao umeshuhudia ghasia siku za hivi karibuni.

Uchaguzi huo ulitarajiwa kuwa wa kwanza wa Bunge la Taifa la Palestina katika kipindi cha miaka 15 na sasa haijulikani utafanyika lini.

Maandamano yamefanyika katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Ghaza kupinga hatua ya Abbas kuakhirisha uchaguzi huo ambao ulikuwa unasubiriwa kwa hamu.

Wakuu wa utawala haramu wa Israel hawakutaka kuona uchaguzi huo unafanyika na kwa msingi huo wamechochea na kuibua ghasia katika eneo la Quds.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*