?>

Hatua mpya za kustawisha uhusiano wa Iran na Kazakhstan

Hatua mpya za kustawisha uhusiano wa Iran na Kazakhstan

Hati tisa za maelewano na waraka wa ushirikiano kati ya Iran na Kazakhstan zimesainiwa hapa Tehran katika hafla iliyohudhuriwa na marais wa nchi hizo mbili.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Rais Kassym-Jomart Kemelevich Tokayev wa Kazakhstan aliwasili mjini Tehran jana Jumapili kwa ziara ya siku moja hapa nchini na alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Iran akiwemo Rais Ebrahim Raisi.

Katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: "Iran na Kazakhstan zinaweza kuboresha zaidi uhusiano wao" na akaongeza kuwa, "mikataba iliyosainiwa leo au siku za nyuma ni ishara muhimu ya nia ya nchi mbili ya kuendeleza uhusiano".

Katika miezi ya karibuni na sambamba na kuongezeka vikao vya mashauriano na mikutano iliyofanywa na viongozi wa Serikali ya 13 ya Iran na wa nchi jirani na za ukanda huu, zimefunguliwa njia nyingi katika uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Kazakhstan.

Kuongezeka uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi mbili kunadhihirisha nia ya dhati ziliyonayo Iran na Kazakhstan ya kupanua na kuimarisha zaidi mashirikiano baina yao. Katika mwaka uliopita wa 1400 wa kalenda ya Iran yalifanyika mabadilishano ya karibu tani 729,000 za bidhaa zenye thamani ya dola milioni 265,200,000, ambayo yakilinganishwa na mwaka wa kabla yake ni ongezeko la asilimia 71 kwa upande wa bidhaa zenyewe na asilimia 29 kwa thamani ya bidhaa hizo.

Misimamo ya Iran na Kazakhstan inakaribiana pia katika masuala ya eneo ikiwemo kadhia ya Afghanistan, ambapo nchi zote mbili zinataka iundwe serikali pana na jumuishi itakayoshirikisha makundi yote ya kisiasa na kikabila ya nchi hiyo. 

Ukiachilia mbali masuala ya kisiasa na mashirikiano ya kikanda, viongozi wa Iran na Kazakhstan wamefanya mazungumzo mazuri pia kuhusiana na kustawisha mashirikiano ya sekta za reli, barabara na anga, ambapo kufikiwa kwa malengo hayo kunaweza kuzifanya pande hizo mbili ziwe na mchango na nafasi athirifu katika eneo.

Mnamo mwezi Septemba mwaka 2021 wakati marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kazakhstan walipokutana pembeni ya mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai uliofanyika nchini Tajikistan, iliafikiwa kwamba ushirikiano baina ya pande mbili ukiwemo wa sekta ya reli ustawishwe zaidi.

Kwa muda wa muongo mmoja sasa, Iran na Kazakhstan zimeliweka katika ajenda kuu ya ushirikiano wao wa kistratejia suala la upitishaji, uchukuzi na usafirishaji wa bidhaa kimataifa. Tangu mwaka 2003, wakati Kazakhstan ilipojiunga na ushoroba wa kimataifa wa Kaskazini-Kusini, ambao Iran ni mmoja wa wanachama wake wakuu; kwa muda wote wa miaka iliyofuatia baada ya hapo nchi hiyo imeonyesha hamu pia ya kuwekeza katika bandari ya kistratejia ya Iran ya Chah Bahar. Mnamo tarehe 18 Mei, mkuu wa bandari ya Aktau nchini Kazakhstan Abai Turikpenbayev alitembelea Chah Bahar na kueleza bayana kwamba: "Ziara yetu imejikita katika suala la utumiaji wa njia za kupitishia bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran".

Kutokana na nafasi ya kistratejia iliyonayo, bandari ya Chah Bahar nchini Iran ni njia ya karibu zaidi ya kufikia eneo la maji ya kimataifa kwa nchi za Asia ya Kati zilizozungukwa na mipaka ya nchi kavu ikiwemo Kazakhstan, Afghanistan, Turkmenistan, Uzbekistan, Tajikistan na Kyrgyzistan.

Kwa upande wa nishati pia, kuna fursa nyingi za ushirikiano kwa Iran na Kazakhstan; na hivi sasa maafisa husika na wataalamu wa nchi mbili wanalifanyia kazi suala la kuendeleza maeneo ya uchimbaji mafuta ghafi na ya LNG, upokeaji na usafirishaji wa mafuta, gesi na bidhaa zitokanazo na mafuta na utoaji huduma za ufundi na uhandisi.

Ni wazi kwamba kutokana na hati zilizosainiwa jana na maafisa wa nchi mbili, fursa mpya zimepatikana za kuongeza na kustawisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja za biashara za pande mbili, upitishaji bidhaa na mazao ya kilimo, nishati pamoja na ushirikiano wa reli kati ya Iran na Kazakhstan.

Rais Kassym-Jomart Kemelevich Tokayev wa Kazakhstan amesema, hati za ushirikiano zilizosainiwa jana zinaweza kupeleka hatua moja mbele maelewano na mashirikiano baina ya nchi mbili na akasisitiza kwamba: Iran na Kazakhstan zina mtazamo mmoja pia katika masuala ya kikanda na kimataifa. Nchi hizi mbili zinakubaliana juu ya kuimarishwa mashirikiano yao katika jumuiya za kikanda na kimataifa na vilevile kuhusiana na kuimarishwa uthabiti na usalama wa eneo.../

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*