?>

Indhari ya UNICEF: Idadi ya watoto wanaokosa masomo kwa sababu ya majanga imeongezeka sana

Indhari ya UNICEF: Idadi ya watoto wanaokosa masomo kwa sababu ya majanga imeongezeka sana

Mfuko wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu elimu kwenye maeneo yenye dharura na majanga, ECW umetoa ripoti ya kutisha ikidokeza kuwa idadi ya watoto wenye umri wa kwenda shule, ambao wameathirika na majanga na hivyo kuhitaji msaada wa kielimu imeongezeka kutoka milioni 75 mwaka 2016 hadi milioni 222 hii leo.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Mkurugenzi wa mfuko huo Yasmine Sherif, amesema, katika idadi hiyo inayojumuisha watoto na barubaru, milioni 78.2 hawako shuleni, milioni 120 wako shuleni lakini hawapati hata kiwango cha chini cha uelewa wa hisabati au kusoma na kwamba idadi hiyo inamaanisha kuwa, ni mtoto 1 kati ya 10 kwenye maeneo hayo ndio ana uwezo wa kufanya hisabati na kusoma. 

Kwa mujibu wa Bi Sharif, asilimia 84 ya watoto hao wanaishi kwenye maeneo yenye mizozo iliyodumu kwa muda mrefu kama vile Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mali, Nigeria, Sudan Kusini, Sudan na Yemen.

Akizungumzia hali hiyo katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, watoto hao milioni 222 kote duniani elimu yao imeingiliwa na kuvurugwa na zaidi ya hapo “ndoto zao za mustkbali bora zimeporwa na vita na kutawanywa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.”

Guterres ameongeza kuwa, katika wakati wa majanga hayo mfuko wa ECW unasimama pamoja na watoto hao walioko katika nchi 40 duniani.

Halikadhalika, Katibu Mkuu wa UN amezitolea mwito serikali, makampuni ya biashara mifuko mbalimbali ya ufadhili na watu binafsi kuunga mkono na kusaidia kazi muhimu inayofanywa na ECW.../342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*