?>

Jeshi la Chad lasema limeua 'mamia ya waasi'

Jeshi la Chad lasema limeua 'mamia ya waasi'

Baraza la kijeshi linalotawala Chad katika kipindi cha mpito limedai kuwa limeua mamia ya waasi katika makabiliano makali ya siku mbili huko mashariki mwa nchi, ambako aliyekuwa rais wa nchi hiyo Idriss Deby aliuawa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Msemaji wa baraza hilo, Azem Bermandoa Agouna amesema katika taarifa kuwa, idadi kubwa ya waasi hao waliuawa baada ya vyombo vya usalama na ulinzi kuanzisha operesheni ya kuyatokomeza makundi ya waasi katika mji wa Nokou, kaskazini mwa eneo la Kanem, umbali wa kilomita 200 kaskazini mwa mji mkuu, N'Djamena.

Bila kutaja idadi kamili, Agouna amesema, "katika operesheni tuliyofanya Aprili 29 na 30, tumefanikiwa kuangamiza mamia ya waasi, huku wengine 66 wakitiwa mbaroni." Msemaji wa Baraza la kijeshi linalotawala Chad amesema wanajeshi sita wa serikali wameuawa pia katika makabiliano hayo.

Tangu katikati ya mwezi uliopita wa Aprili, wanajeshi wa Chad wamekuwa wakikabiliana na waasi wa kundi la FACT, katika eneo la jangwa la Kanem, mpakani na Niger.

Hivi karibuni, Baraza tawala la kijeshi la Chad lilisema halitafanya mazungumzo na waasi hao walioanzisha mashambulio katika eneo la kaskazini ya nchi, wakituhumiwa kumuua Idriss Deby.

Waasi wa kundi la FACT waliingia Chad Aprili 11 kupitia mpaka wa kaskazini wa nchi hiyo wakitokea Libya na wito wa kuhitimisha utawala wa miaka 30 wa Rais Idriss Deby, ambaye aliuawa kabla ya kula kiapo cha kuhudumu muhula wa sita wa uongozi baada ya kushinda uchaguzi wa rais.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*