?>

Jibu la Pakistan kwa msimamo wa India kwamba Kashmir itaendelea kuwa sehemu ya ardhi yake

Jibu la Pakistan kwa msimamo wa India kwamba Kashmir itaendelea kuwa sehemu ya ardhi yake

Mwakilishi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa amepinga msimamo uliotangazwa na India kwamba eneo la Kashmir halitatenganishwa na ardhi ya nchi hiyo na akasisitiza kwa mara nyingine tena kuwa, Jamu na Kashmir haijawahi na wala katu haitakuwa sehemu ya India; na New Delhi haina haki yoyote katika eneo hilo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ni zaidi ya miongo saba sasa wingu la mgogoro wa eneo la Kashmir limegubika uhusiano wa India na Pakistan, ambapo chanzo na chimbuko la mzozo na mvutano baina ya pande hizo mbili linarejea mwishoni mwa muongo wa 1940, wakati lilipoamuliwa suala la kuligawanya eneo la Bara Hindi, maeneo ya Waislamu ya Jamu na Kashmir nayo yaliamuliwa kuwa sehemu ya Pakistan. Lakini kutokana na umuhimu wa kistratejia wa eneo hilo pamoja na hali zake za kipekee za mvuto wa utalii, vikosi vya jeshi la India vikishirikiana na vya Uingereza, vilitumia kisingizio cha ombi lililotolewa na Maharaja wa zama hizo wa Jamu na Kashmir kulishambulia na kuiweka chini ya udhibiti wake sehemu muhimu ya eneo hilo.

"Kuhodhiwa sehemu kadhaa za Jamu na Kashmir na kukwamishwa mpango wa kugawanywa eneo la Bara Hindi ilikuwa ni njama ya Uingereza ambayo ilitaka tofuati na mivutano kati ya India na Pakistan juu ya Kashmir libaki kuwa jeraha bichi lisilo na dawa ili nchi hizo mbili zisiweze kamwe kuwa na uhusiano mzuri kama mataifa mawili jirani."

India na Pakistan zimeshapigana vita mara mbili kugombania umiliki wa eneo la Kashmir; na mnamo mwaka 1999 pia zilikaribia kutumbukia kwenye lindi la vita kamili katika miinuko ya Kargil na kupelekea kufanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Pakistan yaliyomweka madarakani Jenerali Parviz Musharraf.

Kuingia madarakani nchini India chama cha Wahindu cha Bharatia Janata, BJP ambacho kinafuata sera za mielekeo ya Kihindu inayolenga kuyafurahisha na kuyaridhisha makundi ya Kihindu yenye chuki na misimamo ya kufurutu mpaka; na kuendelezwa uungaji mkono wa makundi hayo kwa BJP, hatimaye mnamo mwezi Agosti 2019, kifungu cha 370 cha Katiba ya India ambacho kilikuwa kimelipatia eneo la Jamu na Kashmir hadhi maalumu ya mamlaka ya ndani ya kujiendeshea mambo yake kilifutwa; na hatua iliyofikiwa hivi sasa ni ya India kudai kuwa eneo la Kashmir inalolikalia, litabaki kuwa sehemu ya ardhi ya nchi hiyo na Pakistan haina haki tena juu ya suala hilo.

Hii ni katika hali ambayo, si tu Pakistan inapinga dai hilo la India, lakini inaitakidi pia kwamba, kulingana na azimio la Umoja wa Mataifa, Kashmir ni eneo linalogombaniwa; na kwamba hatima yake inapasa iamuliwe na watu wenyewe wa eneo hilo.

Khalid Rahman, mtaalamu wa masuala ya Ukanda huu aliyeko Pakistan anasema: "bila kutatuliwa mgogoro wa Kashmir, uhusiano wa India na Pakistan hautakuwa wa kawaida; na utumiaji mabavu unaofanywa na India kuhusiana na Kashmir si njia ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo bali ni kuufanya uwe tata zaidi."

Alaa kulli haal, hatua iliyochukuliwa na Bunge la India Agosti 5 2019 ya kubatilisha kifungu cha Katiba kinacholipa eneo la Kashmir inalolikalia hadhi maalumu ya kujiendeshea mambo yake imeifanya hali ya eneo hilo iwe tata zaidi. Sababu ni kwamba kwa muijbu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hali ya Jamu na Kashmir inapasa itatuliwe kwa kura ya maoni ya kuamua hatima ya eneo hilo. Hata hivyo serikali ya India ya chama cha BJP inalipinga suala hilo na badala yake inaendeleza mkakati wa nguvu za mtutu wa bunduki kwa mujibu wa sera zake za ndani huku ikiendelea kuwakamata wa kuwaweka kwenye vizuizi vya nyumbani viongozi wa Kashmir ili kujizatiti na kuimarisha zaidi nafasi yake katika eneo hilo.

Lakini kwa mtazamo wa Pakistan na makundi ya Kashmir, umiliki wa eneo hilo ungali ni suala linalozozaniwa; na sera za India za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja haziwezi kuhitimisha mgogoro wa eneo hilo.../

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*