?>

Juhudi za Uturuki za kujenga kambi za kijeshi kaskazini mwa Iraq

Juhudi za Uturuki za kujenga kambi za kijeshi kaskazini mwa Iraq

Serikali ya Uturuki imezidisha njama na chokochoko za kufanikisha malengo yake ya nje ya mipaka ya Uturuki ambapo sasa imeanza kuzungumzia nia yake ya kuanzisha kambi za kijeshi kaskazini mwa Iraq.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Süleyman Soylu ametangaza nia ya nchi yake ya kujenga kambi ya kijeshi kaskazini mwa Iraq. Vile vile amegusia kambi za kijeshi za Uturuki ndani ya ardhi ya Syria na kusema kuwa, Ankara ina nia ya kuwa na kambi za kijeshi kaskazini mwa Iraq kama ilivyo na kambi hizo nchini Syria ili kudhibiti usalama katika maeneo ya karibu na mipaka ya Uturuki.

Miaka kadhaa nyuma, Uturuki ilifanya mashambulio ndani ya ardhi ya Iraq kwa madai ya kupambana na wanamgambo wa chama cha PKK cha Wakurdi. Mashambulizi ya wanajeshi wa Uturuki kaskazini mwa Iraq yanaendelea katika hali ambayo, muda wote serikali ya Iraq na wananchi wa nchi hiyo wamekuwa wakilalamikia vikali uvamizi huo wa Uturuki katika nchi yao ambao ni kinyume na sheria zote za kimataifa na ujirani mwema. Kwa mfano, Rais Barham Saleh wa Iraq ametoa tamko rasmi kulalamikia uvamizi wa kijeshi wa Uturuki katika ardhi ya Iraq na kusema kuwa huko ni kukanyaga waziwazi haki ya kujitawala ardhi ya Iraq na vielelezo vya ujirani mwema, kama ambavyo ni kinyume cha sheria zote za kimataifa, hivyo amewataka viongozi wa Uturuki wakomeshe uvamizi wao wa kijeshi katika maeneo ya kaskazini mwa Iraq.

Taarifa ya Ikulu ya Iraq imesisitiza kuwa, matatizo ya hivi sasa ya Uturuki yanapaswa kutatuliwa kwa ushirikiano na uratibu wa pande mbili. Baraza la Mawaziri la serikali ya Iraq pia limelaani vikali operesheni za kijeshi za hivi karibuni za Uturuki kaskaizni mwa Iraq. Katika kipindi cha chini ya wiki moja, balozi wa Uturuki mjini Baghdad ameitwa mara mbili katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq kutakiwa kutoa maelezo kuhusu uvamizi wa nchi yake kaskazini mwa Iraq na kufikisha malalamiko makali ya Baghdad kwa viongozi wa Ankara. Kwa upande wa Bunge la Iraq pia; chombo hicho cha kutunga sheria ambacho kina wawakilishi wa matabaka yote ya wananchi wa Iraq kimelaani vikali uvamizi wa Uturuki kaskaizni mwa nchi hiyo. Si hayo tu, lakini pia Kamati ya Usalama ya Bunge la Iraq imeitaka serikali ya Baghdad kufungua mashtaka rasmi mbele ya Umoja wa Mataifa dhidi ya viongozi wa Uturuki kutokana na uvamizi wao wa kijeshi kaskazini mwa Iraq. 

Vile vile wabunge kadhaa wa Iraq wametoa taarifa ya pamoja na kumtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mustafa al Kadhimi achukue hatua za kukabiliana na uvamizi wa Uturuki kaskazini mwa Iraq. Wabunge hao wamemtaka Waziri Mkuu wa Iraq asitishe miamala ya kibiashara na kidiplomasia baina ya Baghdad na Ankara kama sehemu ya kukabiliana na opereseheni za kijeshi za Uturuki kaskazini mwa Iraq. Pamoja na hayo, Waziri Mkuu wa Iraq hadi hivi sasa hajachukua hatua yoyote ya maana ya kukabiliana na uvamizi wa kijeshi wa Uturuki kaskazini mwa nchi hiyo, suala ambalo limezusha hasira za mirengo mbalimbali bungeni. Uzoroteshaji huo wa mambo wa Waziri Mkuu wa Iraq umewafanya baadhi ya wataalamu wa mambo waamini kwamba, operesheni za kijeshi zinazofanywa na Uturuki kaskazini mwa Iraq zinafanyika kwa idhini na baraka za siri za baadhi ya viongozi nchini Iraq.

Ammar al Hakim, kiongozi wa mrengo wa al Hikma katika Bunge la Iraq amezungumzia mashambulio ya hivi karibuni ya Uturuki kaskazini mwa Iraq na kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Kwa miongo mingi sasa Wairaq wanajitolea muhanga kila kitu chao kwa ajili ya kulinda uhuru na haki ya kujitawala taifa lao. Tunalaani njama zozote za kukanyaga haki ya kujitawala Iraq kutoka nchi yoyote ile. Serikali ya Baghdad nayo ina wajibu wa kuchkua hatua zinazotakiwa kuzilazimisha nchi zote jirani hasa Uturuki ziheshimu haki ya kujitawala ardhi yote ya Iraq.

342/
Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*