?>

Katibu Mkuu wa UN: Jamii ya kimataifa ishughulikie changamoto za kaskazini mwa Nigeria

Katibu Mkuu wa UN: Jamii ya kimataifa ishughulikie changamoto za kaskazini mwa Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema jamii ya kimataifa inapaswa kutambua changamoto kubwa zinazolikabili jimbo la kaskazini mashariki mwa Nigeria la Borno, ambazo ni pamoja na ugaidi ili kurejesha hali ya matumaini katika eneo hilo ambalo limekuwa likishuhudia ugaidi ambao umesababisha watu wengi wawe wakimbizi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: António Guterres ametoa wito huo baada ya kutembelea kituo kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa cha kuwajumuisha katika jamii watoto ambao wamejihusisha na makundi yenye silaha, huko Maiduguri, mji mkuu na mji mkubwa zaidi wa Jimbo la Borno. 

Jimbo la Borno limekuwa moja wapo ya vitovu vya itikadi kali na shughuli za kigaidi nchini Nigeria na katika eneo zima la Sahel. Jimbo hilo linatajwa kuwa ngome ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Ukosefu wa usalama katika kipindi cha miaka 12 iliyopita unaohusishwa na makundi yenye silaha, likiwemo kundi la kigaidi la Boko Haraam, umeathiri maisha na kusababisha takriban watu milioni 2.2 kuyahama makazi yao, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. 

Wengi wa watoto hao walilazimishwa au kuchaguliwa, kwa kukosa fursa nyingine, kujiunga na vikundi vya kigaidi na kuchukua silaha kama wapiganaji. Wengine waliwekwa kizuizini na kisha kuachiliwa baada ya kushukiwa kuhusika na vitendo vya ghasia na machafuko.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa mahitaji ya kibinadamu kaskazini-mashariki mwa Nigeria yanaendelea kuwa makubwa, yakichangiwa na janga la COVID-19 na kuzorota kwa hali ya uhakika wa chakula, kutokana na changamoto zinazowakabili wakulima katika kuzalisha na kuuza mazao. 

Guterres ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa "kuwekeza ili kurejesha matumaini Borno, kutoa msaada kwa miradi ya serikali ya Borno na mashirika ya kiraia ili kuunda mazingira ya maendeleo ya kweli, mazingira ambayo shule zinafanya kazi, hospitali zinafanya kazi na ajira zipo; hali ambayo watu wanaweza kuishi kwa amani na mshikamano.” 

Pia amesema jamii ya kimataifa inahitaji kuunga mkono "si tu hali ya matumaini, bali hali bora ya maisha  ambayo itaangamiza ugaidi." 342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*