?>

Kikao cha Tehran na mustakbali wa Afghanistan

Kikao cha Tehran na mustakbali wa Afghanistan

Kikao cha makundi ya Kiafghani ambacho kimefanyika hapa Tehran siku za Jumatano na Alhamisi kikihudhuriwa na wawakilishi wa serikali ya Afghanistan, shakhsia na ujumbe wa kisiasa wa ngazi ya juu wa kundi la Taliban chini ya uwenyeji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kilimaliza shughuli zake kwa kutolewa taarifa yenye vipengee sita.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hapa tunaweza kuashiria nukta kadhaa kuhusu matokeo ya kikao cha Tehran na matarajio ya baadaye ya Afghanistan. 

Nukta ya kwanza ni kuwa, makundi ya Kiafghani yameshukuru na kupongeza kufanyika kikao hicho ambacho kimedhihirisha juhudi na nia njema ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenye shabaha ya kurejesha amani huko Afghanistan. Aghalabu ya weledi wa mambo wanaamini kuwa, Iran ni kati ya nchi muhimu katika eneo hili na inaweza kutumia ushawishi wake mkubwa kuainisha mwelekeo wa matukio ya baadaye ya Afghanistan. Kufanyika kikao cha siku mbili hapa Tehran kuhusu hali ya usalama wa Aghanistan kwa upande mmoja kunadhihirisha umuhimu wa matukio ya nchi hiyo kwa Iran; na kwa upande mwingine kunaonyesha namna Tehran inavyotilia maanani amani na usalama katika eneo hili. 

Nukta ya pili ni kuwa, kwa mtazamo wa makundi ya Waafghani yaliyoshiriki katika kikao cha siku mbili cha Tehran, vita si suluhisho la matatizo ya Afghanistan, na kwamba njia pekee ya kuondokana na machafuko ya sasa nchini humo ni kufanya jitihada za kupata ufumbuzi wa kisiasa na wa amani kwa matatizo ya nchi hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, makundi yaliyoshiriki katika kikao cha Tehran yamekubaliana kwamba, njia ya ufumbuzi wa kisiasa ndiyo njia pekee itakayoiwezesha Afghanistan kujikwamua katika hali ya ukosefu wa amani na machafuko. Kwa sababu hiyo, makundi yaliyoshiriki katika kikao cha Tehran yamekubaliana kujadili na kufikia natija kuhusu masuala yote yanayohitaji mashauriano zaidi kama kuanzisha mfumo wa kutoka katika kipindi cha vita kuelekea katika amani ya kudumu, kuhusu mfumo wa Kiislamu unaokubalika na pande zote na namna ya kuundwa kwake.  

Nukta nyingine ni kuwa, makundi ya Kiafghani yaliyohudhuria kikao cha Tehran yanaamini kuwa, kikao hicho ni fursa na uwanja mpya wa kuboresha juhudi za kutafuta utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Afghanistan. Makundi hayo yamesisitiza suala la kuboreshwa ufumbuzi wa kisiasa ili kutatua masuala ya Afghanistan katika hali ambayo licha ya kufikiwa mapatano ya Doha lakini mapigano ya ndani nchini humo yameongezeka sambamba na kuondoka nchini humo wanajeshi vamizi wa nchi za Magharibi. Zaidi ya hayo ni kwamba, mazungumzo kati ya makundi ya Kiafghani yalianza katika mwezi wa Kiirani wa Shaharvar mwaka jana huko Qatar; hata hivyo mazungumzo hayo hayakuwa na matunda ya kuridhisha na mikutano ya pande mbili imesitishwa kwa miezi kadhaa sasa. 

Nukta ya nyingine muhimu ni kuwa, kama ilivyoashiriwa, mapigano ya ndani yameshtadi huko Afghanistan katika miezi ya karibuni. Mapigano yameongezeka nchini humo katika hali ambayo, nchi za Magharibi hususan serikali za Marekani na Uingereza kama waonavyo aghalabu wa weledi wa masuala ya kisiasa, zinawaondoa wanajeshi wao huko Afghanistan katika hatua inayotajwa kuwa si ya kuwajibika. Rais Joe Biden wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson,  siku ya Alhamisi iliyopita walitangaza kuwa, wanajeshi wa nchi zao waliosalia Afghanistan watakuwa wameondoka nchini humo hadi kufikia Septemba 11. Nukta ya kushangaza zaidi hapa ni kuwa, Rais wa Marekani alitangaza kwamba, muda wa kuhudumu wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan unamalizika rasmi tarehe 31 Agosti na kudai kuwa, Marekani imefikia malengo yake huko Afghanistan! Biden ametaja masuala kama eti kuendesha vita dhidi ya magaidi ambao walitekeleza shambulio dhidi ya Marekani Septemba 11 mwaka 2002, kumuadhibu Usama bin Laden na eti kuzuia kubadilishwa Afghanistan na kuwa kituo cha kutekelezea mashambulizi dhidi ya Marekani kuwa ndio yaliyokuwa malengo makuu ya kuwepo majeshi ya nchi hiyo huko Afghanistan kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.  

Viongozi wa serikali ya Marekani wanatoa matamshi ya kuhalalisha hatu ya kuondoka wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan katika hali ambayo kwa upande mmoja vita vya ndani kati ya Taliban na serikali ya Afghanistan vimeongezeka; na kwa upande wa pili, kuondoka Afghanistan wanajeshi vamizi wa Marekani na wa nchi nyingine ajinabi katika hali ya hivi sasa kutazidisha vita nchini humo. Kuhusiana na suala hilo rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai anasema: "Hali ya sasa ya Afghanistan ni matokeo ya kufeli na kushindwa Marekani. Marekani imefeli katika kupambana na ugaidi. Afghanistan ilivyo sasa si nchi iliyoshindwa kwa sababu wtu wake walibuni katiba mpya, wakashiriki katika uchaguzi na kukumbatia demokrasia. Ama muungano wa nchi ajinabi chini ya uongozi wa Marekani umefeli na kushindwa katika kutekeleza majukumu yake nchini Afghanistan." 

Nukta nyingine ni kuwa, Marekani na Uingereza zimetangaza kuwaondoka wanajeshi wao huko Afghanistan katika hali ambayo, kwa mtazamo wa weledi wa mambo, kuondoka kwa vikosi vamizi vya Marekani nchini Afghanistan kunaandamana na kufeli pakubwa. Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia anasema: "Kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan ni sawa na kukiri Washington kwamba imefeli na kushindwa nchini humo."  

Mbali na matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, aghalabu ya wabunge wa Afghanistan pia wamewakosoa viongozi wa Marekani na kuutaja utendaji wa miongo miwili wa Washington nchini humo kuwa uliofeli. Kuhusiana na suala hilo, Hamidullah Hanif mbunge wa jimbo la Herat katika Bunge la Afghanistan anasema: "Kuibua machafuko na hitilafu za kikabila, kuzidisha ufisadi wa kiidara, kuongezeka kilimo na magendo ya madawa ya kulevya, mauaji na utekaji nyara, kujikariri masuala ya wahajiri, kuifanya Afghanistan ishindwe kujiendeshea masuala yake yenyewe ni kati ya matunda ya miongo miwili ya kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan." 

Kwa ujumla tunapasa kusema kuwa, hatua ya Tehran ya kuwa mwenyeji wa kikao cha makundi ya kisiasa ya Afghanistan inadhihirisha kwamba, Iran inatilia maanani na kuunga mkono suala la kujitawala, mamlaka ya kitaifa, utulivu, amani na usalama wa majirani zake ikiwemo Afghanistan, na katika upande mwingine, Iran na nchi nyingine za kanda hii zinaunga mkono juhudi za viongozi wa Afghanistan za kurejesha amani, utulivu na maendeleo kwa wananchi wa nchi hiyo. 

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*