?>

Kiongozi Muadhamu: Uchaguzi wa rais nchini ulifanyika kwa hamasa kubwa

Kiongozi Muadhamu: Uchaguzi wa rais nchini ulifanyika kwa hamasa kubwa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo amesema kuwa wananchi wa Iran ndio washindi halisi wa uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi huu katika mazingira ya maambukizi ya corona na matatizo ya kiuchumi na kwamba wamemfanya adui na vibaraka wake washindwe na kufeli.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika hadhara ya Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran na maafisa wa chombo hicho waliokwenda kukutana naye kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Idara ya Mahakama. Amesema harakati kubwa za maelfu ya vyombo vya propaganda vikiwemo vyombo vya habari vya Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi tegemezi, na vilevile baadhi ya vibaraka wao wa ndani ya nchi kwa ajili ya kuwazuia wananchi wasishiriki katika zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa rais hazina kifani katika dunia ya sasa. Ameongeza kuwa: Maadui hao walitumia vibaya baadhi ya visingizio kama matatizo ya kimaisha au baadhi ya matukio yaliyotokea baadaye kama suala la kupasisha wagombea kwa ajili ya kutimiza njama zao.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kadhia ya virusi vya corona na jinsi maambukizi ya virusi hivyo yalivyopunguza karibu asilimia 10 ya wapiga kura kwa mujibu wa tathmini ya wataalamu wa mambo na kusema: Licha ya matatizo hayo yote wananchi walitengeneza hamasa kubwa na halisi kwa kusimama kwenye safu ndefu za kupiga kura tangu mapema asubuhi na hivyo wakatoa kipigo kikali kwa wale waliosusia zoezi hilo na wapinzani wa uchaguzi. 

Ameyataja baadhi ya matukio yaliyoshuhudiwa katika uchaguzi wa rais hapa nchini kuwa yanatoa ibra na mafunzo akisema: Kumeshuhudiwa dhuku na mitazamo tofauti katika midahalo ya wagombea, lakini wagombea wote, tofauti na matakwa ya adui, wameafikiana kwamba, matatizo ya kiuchumi yaliyopo hapa nchini yanaweza kupatiwa ufumbuzi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais nchini Marekani na matusi ya wenyewe kwa wenyewe baina ya wagombea katika midahalo ya uchaguzi huo na kusema: Wamarekani si vigezo bora vya kuigwa; kwa msingi huo kuna ulazima wa kuchunga adabu na masuala ya kimaadili na kisheria katika masuala ya kisiasa na kuzungumza bila ya kuvunjiana heshima na bila ya kutumia mbinu ya matusi na utovu wa maadili ya Kimarekani na ya Donald Trump.

Ayatullah Khamenei amashiria matamshi ya afisa mmoja wa serikali ya Washington kuhusu uchaguzi wa rais nchini Iran na kusema: Uchaguzi wa rais wa Marekani ulijaa fedheha mbele ya macho ya walimwengu na sasa wale waliotengeneza fedheha hiyo wamejitokeza miezi kadhaa baadaye na kuanza kukosoa uchaguzi wa rais wa Iran; baada ya fedheheha ya uchaguzi wa Marekani maafisa wa serikali ya nchi hiyo hawakupaswa tena kutoa hata neno moja kuhusiana na chaguzi zinazoanyika katika nchi nyingine.  

Ayatullah Khamenei ameashiria jinai kubwa iliyofanywa na kundi la kigaidi la MKO ya kumuua shahidi Ayatullah Muhammad Beheshti na maafisa wengine karibu 70 wa Jamhuri ya Kiislamu katika shambulizi la kigaidi na kusema: Magaidi hao walikiri waziwazi kwamba, ndio waliotenda jinai hiyo lakini hii leo wanafanya shughuli zao kwa uhuru na kwa uungaji mkono na himaya ya Ufaransa na nchi nyingine zinazodai kutetea haki za binadamu. Amesisitiza kuwa, fedheha hiyo ya Wamagharibi katika madai ya kutetea haki za binadamu na kuwapa jukwaa na kuwaunga mkono magaidi hao vinawaweka wanadamu katika tahayuri na kuwaacha bumbuazi.  

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*