?>

Kuendelea mtikisiko katika soko la nishati, Russia yaikatia gesi Ufaransa

Kuendelea mtikisiko katika soko la nishati, Russia yaikatia gesi Ufaransa

Huku vita vya Russia na Ukraine vikiendelea na vikwazo vya nchi za Magharibi kuwekewa Moscow, mauzo ya gesi ya Russia kwa Ulaya yamepungua sana na kuziacha nchi nyingi za bara hilo zikikumbwa na tatizo la kujidhaminia nishati na kuongezeka gharama ya bidhaa hiyo muhimu.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Kuhusiana na hilo, shirika la gesi la Gazprom la Russia limetangaza kupunguza kwa asilimia 50 mauzo ya gesi kwenda Italia. Mtiririko wa gesi katika mitandao ya usambazaji wa nishati kwa nchi zingine za Ulaya pia umekatishwa. Katika uwanja huo, vyanzo vya Kifaransa vimethibitisha kwamba nchi hiyo haijapokea gesi kutoka Russia kupitia bomba. Kampuni ya Usafirishaji wa gesi ya Ufaransa GRTgaz imesema kuwa mtiririko wa gesi ya Russia kupitia Ujerumani umesitishwa na kwamba nchi hiyo haijapokea gesi yoyote kutoka Russia kupitia bomba hilo tangu Juni 15. Hii ni katika hali ambayo Ufaransa ambayo inategemea sana nishati ya Russia  inadhamini takriban asilimia 17 ya gesi inayotumia kupitia mtandao uliounganishwa na Ujerumani.

Mapema wiki hii, Gazprom ilionya kwamba itapunguza kwa kiasi kikubwa usambazaji wa gesi kwa Ulaya kutokana na masuala ya kiufundi yanayotokana na vikwazo vya Magharibi. Gazprom inahusisha masuala hayo na ucheleweshaji unaofanywa kwa makusudi na shirika la Ujerumani la Siemens, ambalo limejiunga na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia. Kwa hakika vikwazo hivyo vimezuia kupatikana vifaa muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya kuendeshea operesheni ya bomba la gesi la Nord Stream. Kwa hivyo, usambazaji wa gesi ya Russia kwenda Ulaya kupitia bomba hilo umepungua kwa asilimia 60 wiki hii, na hivyo kusababisha bei ya gesi barani Ulaya kupanda sana.

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, na kufuatia kuanza vita vya Russia na Ukraine nchi za Ulaya zimebuni na kutekeleza vifurushi mbalimbali vya vikwazo kwa ajili ya kutoa mashinikizo dhidi ya Russia. Lakini vikwazo hivyo sasa vimefanya mambo kuwa magumu kwa nchi za Ulaya zenyewe, ambazo zinategemea sana rasilimali za nishati za Russia. Bei ya mafuta barani Ulaya imepanda kwa kasi kubwa na hivyo kusababisha bei za bidhaa na huduma nyingi kupanda, huku nchi nyingi za bala hilo zikikabiliwa na mfumuko wa bei na kushuka kwa ukuaji wa uchumi. Bei ya saa moja ya megawati ya gesi asilia katika masoko ya Ulaya, imefikia euro 130. Hii ni katika hali ambayo bei hiyo wiki iliyopita ilikuwa euro 100 na mwaka uliopita euro 30.

Sunstone mwanauchumi wa ngazi za juu wa Ulaya anasema katika uwanja huo kwamba: Kuwekewa vikwazo kamili mabomba ya gesi yanayoingia Ulaya kutoka Russia kumepunguza pato la taifa la kanda ya euro kwa asilimia 2.2 mwaka huu wa 2022.

Maafisa wa Russia awali walionya kwamba vikwazo vya nishati, pamoja na kuondolewa bima meli za mizigo na biashara za nchi hiyo, kungeongeza pakubwa bei ya bidhaa, kuibua msukosuko katika soko la nishati na kuvuruga ugavi wa bidhaa hizo. Pamoja na hayo lakini, nchi za Ulaya bado zinaendelea na sera yao ya vikwazo dhidi ya Russia ambapo tarehe 2 Juni ziliidhinisha kifurushi cha sita cha vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

Christine Colemann, Mkuu wa Muungano wa Viwanda vya Kemikali vya Ujerumani, huku akiashiria hasara kubwa inayoweza kupata Ujerumani iwapo uagizaji wa gesi ya Russia utapigwa marufuku amesema kupigwa marufuku kabisa gesi ya nchi hiyo si jambo la mantiki na ni upumbavu mtupu.

Hii ni katika hali ambayo licha ya kuwa ni majira ya joto na nchi za Ulaya hazikabiliwi na uhaba mkubwa wa gesi, lakini bila shaka mwaka huu nchi hizo haziwezi kufanya mambo yao kama zilivyofanya mwaka uliopita. Kila mwaka, nchi za Ulaya hutumia msimu wa kiangazi kujaza akiba zao ili zisikose nishati wakati wa msimu wa baridi.

Nchi za Ulaya zinatafuta vyanzo mbadala vya kukidhi mahitaji yao ya nishati, huku wachambuzi wakisema kukata kabisa utegemezi wa bara hilo kwa gesi ya Russia ni mchakato utakaochukua muda mrefu na kwa uchache utaendelea hadi mwaka 2024. Vikwazo vinaonekana kuwa na athari mbaya kwa nchi za Ulaya, na hasa kwa uchumi wao, badala ya kuiathiri Russia, suala ambalo viongozi wa Ulaya wanalikiri wazi na wana wasiwasi mkubwa nalo.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*