?>

Kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, changamoto ya dunia nzima

Kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, changamoto ya dunia nzima

Tabia ya baadhi ya madola ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja (unilateralism) sasa imekuwa tishio katika upeo wa kimataifa, na njia ya kukabiliana na tishio hilo ni hatua shirikishi na za pamoja katika upeo wa dunia nzima na kuimarisha utamaduni wa kuchukua maamuzi shirikishi (multilateralism) hususan katika masuala ya kimataifa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Muhammad Javad Zarif ambaye jana alihutubia mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama katika Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) kwa njia ya video, alisisitiza udharura wa kukabiliana na changamoto hiyo. 

Ukweli ni kwamba, tabia ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ni tishio lenye taathira haribifu kwa nchi zote na kwa mahusiano ya kimataifa. Kwa maneno mengine ni kuwa, sera za Marekani za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja kuhusiana na masuala ya kimataifa zimesababisha matatizo mengi kwa jamii ya kimataifa. Kuziwekea vikwazo nchi mbalimbali, kutishia kutumia mabavu, kuingilia kijeshi katika nchi nyingine na kujiondoa katika mikataba na makubaliano ya kimataifa ni miongoni mwa hatua zinazokiuka kanuni na sheria za kimataifa.

Alexandre Austin mchambuzi na mwandishi Mfaransa wa kitabu cha "Vikwazo Ilivyotishwa Iran na Taathira Zake Haribifu" (Des sanctions imposees a l'iran et de leurs effets) anasema kuwa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani ni miongoni mwa vielelezo vya sera za kibeberu za serikali ya Washington na kuongeza kuwa: Vikwazo vya Marekani vimekuwa sababu ya kukanyagwa haki za mataifa kama Iran, Venezuela na Cuba. Kwa sababu hiyo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja kutokana na athari zake mbaya.."

Ni wazi kuwa, kimya cha nchi nyingine mbele ya hatua kama hizo za kijuba kina madhara na taathira mbaya, sawa kabisa na sera zenyewe za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja. Hii ni kwa sababu, katika kipindi cha muda mrefu, kimya hicho kitapelekea kupuuzwa na kukanyagwa sheria za kimataifa. Kwa msingi huo, jamii ya kimataifa inalazimika kupinga sera hizo na kuunga mkono utawala wa sheria. 

Hotuba iliyotolewa na Zarif katika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa NAM imeashiria nukta mbili muhimu katika uwanja huu ambazo iwapo zitatiliwa maanani zinaweza kuimarisha sera za kuchukua maamuzi kwa pamoja na shirikishi kuhusiana na masuala ya kimataifa.

Nukta ya kwanza ni udharura wa kutiliwa maanani athari mbaya za sera na utamaduni wa kujichukulia maamuzi ya upande mmoja bila ya kuzingatia maoni na mitazamo ya pande nyingine; jambo ambayo lina madhara kwa jamii nzima ya dunia. Hivyo kuna udharura wa kupinga na kukabiliana na sera hizo.

Nukta ya pili ni udharura wa jamii ya kimataifa kulinda haki zake mbele ya sera za kijuba na za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani. Kuhusiana na suala hili Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema: Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote inaweza kutayarisha fursa na mazingira mazuri zaidi kwa ajili ya kuimarisha sera za kuchukua maamuzi shirikishi na ya pande kadhaa mkabala wa maamuzi ya upande mmoja na ya kijuba katika medani ya kimataifa.

Kwa sasa ni kweli kwamba jamii ya kimataifa inakabiliana na changamoto nyingi ambazo hazijawahi kushuhudiwa, na nyingi kati ya changamoto hizo zinatokana na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani. Kwa sababu hiyo wasiwasi wa jamii ya kimataifa kuhusiana na sera hizo za Washington umeongezeka maradufu.

Katika uwanja huu tunaweza kuashiria maamuzi ya Marekani ya kutekeleza sheria zake za ndani nje ya nchi hiyo, kupuuza na kukanyaga sheria za kimataifa, kueneza misimamo ya kuchupa mipaka kwa malengo ya kisiasa na kuunga mkono tawala za kigaidi sambamba na kutambua rasmi unyakuzi wa ardhi za nchi nyingine unaofanywa na utawala haramu wa Israel.

Msimamo wa Marekani wa kukanyaga makubaliano ya nyuklia ya JCPOA pia ni mfano mwingine wa siasa za kujichukulia maamuzi ya kijuba na ya upande mmoja za serikali ya Washington.

Kwa kutilia maanani hayo yote inatupasa kusema kuwa, uchukuaji wa maamuzi shirikishi si moja kati ya machaguo kadhaa, bali ndiyo chaguo pekee la jamii ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana ipasavyo na changamoto na migogoro ya dunia ya sasa.    

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*