?>

Kuongezeka mivutano baina ya Russia na Umoja wa Ulaya

Kuongezeka mivutano baina ya Russia na Umoja wa Ulaya

Mivutano baina ya Russia na Umoja wa Ulaya imeongezeka sana hivi sasa. Kuwekeana vikwazo viongozi wa kisiasa wa pande mbili ni silaha kuu inayotumiwa na pande hizo kuonesha ukubwa wa mivutano hiyo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imechukua hatua ya kulipiza kisasi cha kuwekewa vikwazo raia na maafisa wake, kwa kuwawekea vikwazo na kuwaingiza kwenye orodha yake nyeusi, Spika wa Bunge la Ulaya, David Sasuli na maafisa wengine saba wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na wawakilishi wa taasisi rasmi za umoja huo.

Baada ya kuchukuliwa hatua hiyo, taasisi zote za Umoja wa Ulaya zimetoa tamko la pamoja la kulalamikia hatua hiyo ya Russia na kusema kuwa imechukuliwa bila ya hoja za msingi kwa sababu imeulenga moja kwa moja Umoja wa Ulaya. 

Ijapokuwa mivutano baina ya Umoja wa Ulaya na Russia iliongezeka mwaka 2014, hata hivyo mivutano hiyo imeongezeka vibaya mno tangu alipoingia madarakani rais mpya huko Marekani, Joe Biden, kiasi kwamba tunaweza kusema kuwa uhusiano wa pande mbili za Umoja wa Ulaya na Moscow haujawahi kuwa mbaya kiasi chote hiki katika historia.

Kitendo cha Umoja wa Ulaya cha kumuunga mkono Alexei Navalny, mpinzani mkuu wa Rais Vladimir Putin wa Russia na mgogoro wa Ukraine ambapo Ulaya inawaunga mkono wafuasi wa Magharibi nchini humo, eneo ambalo ni muhimu sana kwa Russia, ni miongoni mwa sababu za kuongezeka kupindukia mivutano baina ya Russia na Umoja wa Ulaya hivi sasa.

Uingiliaji wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya ndani ya eneo hilo, hatua za nchi wanachama wa umoja huo za kuiwekea vikwazo Russia na uingiliaji wao wa kijeshi huko Ukraine ni nyezo zinazotumiwa na nchi za Magharibi kuishinikiza Moscow. Vile vile nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya kama vile Poland na Jamhuri ya Czech zimeamua kuwafukuza maafisa wa Russia katika nchi hizo, masuala ambayo yameilazimisha Moscow nayo kuchukua hatua za kulipiza kisasi.

Naam, hatua hizo za nchi za Magharibi zimekumbwa na majibu makali kutoka Moscow. Russia imewafukuza nchini humo wanadiplomasia mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na hatua ya karibuni kabisa ni kuwaweka maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya akiwemo Spika wa Bunge la Ulaya na maafisa wengine 7 wa umoja huo, katika orodha yake nyeusi. 

Kuongezeka mivutano baina ya Umoja wa Ulaya na Russia kuna madhara ya kiuchumi pia. Bunge la Ulaya limepasisha azimio la kutaka Russia iwekewe vikwazo vipya na itolewe katika mtandao wa mabadilishano ya fedha wa SWIFT, hatua ambayo bila ya shaka yoyote itakwamisha mradi wa bomba la gesi ya Russia kuelekea Ulaya maarufu kwa jina la Nord Stream 2. Bomba hilo la gesi litakapomalizika kujengwa, litashusha mno bei ya gesi katika nchi za Ulaya.

Mivutano baina ya Umoja wa Ulaya na Moscow imeongezeka mno hivi sasa katika hali ambayo, mzozo wa kisisa baina ya Russia na Marekani nao ni mkubwa kiasi kwamba hadi hivi sasa serikali ya Joe Biden huko Marekani imeshaiwekea Moscow vikwazo vya kila namna. Inavyoonekana ni kuwa, nchi za Ulaya na Marekani zinabadilisha zamu katika kutoa mashinikizo na kuweka vikwazo. Sasa hivi inaonekana ni zamu ya nchi za Ulaya kushadidisha vikwazo vyao dhidi ya Russia ili kuonesha kuwa ni waitifaki watiifu kwa Marekani. Tab'an wataalamu wa mambo wanasema kuwa, nchi za Ulaya ndizo zitakazodhurika zaidi iwapo mivutano itaendelea baina yao na Russia. Hasa kwa kuzingatia kuwa, mara zote Marekani imekuwa ikiwaacha njiani waitifaki wake kila inapoona 'maji yamezidi unga' na haisiti hata kidogo kutafuta muitifaki mwingine wakati wowote inapoona manufaa yake binafsi yako hatarini.

Vile vile nchi za Ulaya ziko karibu zaidi na Russia kijiografia kuliko Marekani, madhara yoyote ya nchi za eneo hilo, lazima yataziathiri nchi zenye mipaka ya pamoja. Hivyo wachambuzi wa mambo wanasema, si jambo la busara kwa nchi za Ulaya kuvuruga uhusiano wao na jirani yao Russia kwa madai ya kuwa ni waitifaki wa Marekani nchi ambayo katika historia yake yote imethibitisha mara chungu nzima kuwa haina mwamana.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*