?>

Miji 94 kati ya 100 yenye kiwango cha juu zaidi cha uchafuzi wa hewa iko India, China na Pakistan

Miji 94 kati ya 100 yenye kiwango cha juu zaidi cha uchafuzi wa hewa iko India, China na Pakistan

Imeelezwa kuwa kati ya miji 100 inayoongoza kwa uchafuzi wa hewa duniani, 94 kati yao iko katika nchi tatu za Asia za India, China na Pakistan.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Uchunguzi uliofanywa kuhusu hali ya uchafuzi wa hewa duniani unaonyesha kuwa, katika mwaka 2020 miji 46 ya India, 42 ya China na sita ya Pakistan ilikuwa kwenye orodha ya miji100 inayoongoza kwa uchafuzi wa hewa.

Miji mingine sita ni minne ya Bangladeh huku Indonesia na Thailand kila moja ikichangia mji mmoja kwenye orodha hiyo ya miji yenye kiwango cha juu cha uchafuzi wa hewa duniani.

Uchunguzi huo aidha unaonyesha kuwa, katika mwaka 2019 uchafuzi wa hewa ulisababisha vifo vya watu milioni moja na laki saba nchini India.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kati ya miji 20 yenye kiwango cha juu zaidi cha uchafuzi wa hewa, 15 kati yao iko India na akthari yao ni katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo. Imeelezwa kuwa uchomaji nyasi unaofanywa na wakulima katika mashamba unashamirisha uchafuzi wa hewa katika misimu ya mapukutiko na baridi kali. Moshi mchafu wa vyombo vya usafiri, wa viwandani na ule unaotokana na uchomaji taka, nao pia unachangia hali hiyo kwa kiwango cha juu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, watu wapatao milioni saba hufariki dunia kila mwaka kutokana na janga la uchafuzi wa hewa. Aidha zaidi ya asilimia 90 ya watu duniani wanaishi kwenye maeneo yenye kiwango cha juu zaidi cha uchafuzi wa hewa kuliko kilichowekwa na shirika hilo.

Uchafuzi wa hewa unahusishwa pia na maradhi mbalimbali yakiwemo ya pumu, moyo na kisukari.../342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*