?>

Mkutano wa Rais wa Syria na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mkutano wa Rais wa Syria na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, muqawama na kusimama imara wananchi na serikali ya Syria na ushindi waliopata katika vita vya kimataifa, vimeandaa mazingira ya kuongezeka itibari na heshima ya nchi hiyo; na akatilia mkazo kustawishwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Syria.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo jana katika mazungumzo na Rais Bashar al-Assad wa Syria na ujumbe aliofuatana nao.

Katika safari yake hiyo ya siku moja hapa mjini Tehran, Rais Assad wa Syria, akiwa ameandamana na mwenyeji wake Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jana asubuhi alikutana na kufanya mazungumzo na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei amegusia mafanikio makubwa iliyopata Syria kwenye medani za kisiasa na kijeshi na akasema: Syria ya leo, si Syria ya kabla ya vita. Ingawa kabla ya vita miji haikuwa imeharibiwa kama ilivyo hivi sasa lakini heshima na itibari ya Syria sasa hivi ni kubwa zaidi kuliko huko nyuma na nchi zote hivi sasa zinaitazama nchi hiyo kwa jicho la dola lenye nguvu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza pia kwamba, leo hii rais na wananchi wa Syria wanaheshimika mbele ya mataifa ya eneo; na akaongezea kwa kusema: "leo hii baadhi ya viongozi wa nchi majirani zetu sisi na nyinyi wanaitisha vikao na kukutana na viongozi wa utawala wa Kizayuni na kunywa nao kahawa, lakini wananchi wa nchi hizo hizo walijitokeza kwa wingi barabarani katika Siku ya Kimataifa ya Quds na kuulaani utawala wa Kizayuni wa Israel; na hii ndio hali halisi ya eneo hii leo."

Kwa upande wake, Rais Bashar al Assad wa Syria ameshukuru misimamo na uungaji mkono wa taifa na serikali ya Iran na pia amemuenzi Shahid Soleimani na kusema: kusimama imara Iran na kuonyesha misimamo thabiti katika kipindi cha miongo minne iliyopita kuhusiana na masuala ya eneo hili hususan kadhia ya Palestina, kumewathibitishia watu wote wa eneo hili kwamba njia ya Iran ndiyo njia sahihi na ya msingi.

Bashar al-Assad amemueleza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: "vilivyoharibiwa na vita vinaweza kujengwa upya, lakini kama usuli na misingi itatoweka haitawezekana kuijenga tena; na kusimama imara taifa la Iran juu ya usuli na misingi iliyoasisiwa na Imam Khomeini (MA), ambayo imeendelezwa kwa hima yako kumeandaa mazingira ya kupata ushindi mkubwa na wa mara kadhaa taifa la Iran na wananchi wa eneo, hususan wananchi wa Palestina."

Tangu mwaka 2011, wakati Syria ilipoingia vitani kupambana na makundi ya kigaidi na ya ukufurishaji, hii ni mara ya pili kwa rais wa nchi hiyo kufanya safari ya kuja nchini Iran. Safari ya kwanza ya Bashar al-Assad mjini Tehran ilifanyika tarehe 25 Februari 2019 baada ya ushindi uliopata muungano wa Iran, Russia na Syria wa kuwasambaratisha magaidi wa kitakfiri na kurejesha utulivu kwa kiwango fulani nchini Syria.

Kutokana na Syria kuwa sehemu ya kambi ya Muqawama na nafasi yake ya kijiopolitiki, kuanzia Januari 2011, nchi hiyo iliandamwa na hujuma za magaidi wa ukufurishaji. Lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni ngome ya uthabiti na usalama katika Asia Magharibi ilifanya jitihada mbalimbali zikiwemo za kutoa ushauri wa kijeshi ili kuwasaidia wananchi na serikali ya Syria katika vita na magaidi walioandaliwa na Marekani na utawala wa Kizayuni pamoja na maadui wa Muqawama.

Katika kukabiliana na hujuma za maajinabia na vita vikubwa vilivyozishirikisha nchi nyingi za eneo dhidi ya Syria, Iran ilitoa mchango mkuu katika ushindi iliopata nchi hiyo. Washauri wa kijeshi wa Iran na makamanda wake kadhaa akiwemo kamanda Shahidi Qassem Soleimani walipambana bega kwa bega na jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Syria; na hatimaye nchi hiyo ikaweza kusimama imara katika kukabiliana na magaidi na maadui zake.

Katika mazungumzo na rais wa Syria, Kiongozi Muadhalmu wa Mapinduzi ya Kiislamu alimzungumza kwa kumuenzi Shahidi kamanda Qassem Soleimani na akasema: Shahidi huyo mtukufu alikuwa na taasubu maalumu juu ya Syria na alijitolea mhanga kwa maana halisi ya neno hilo, kiasi kwamba hatua alizochukua nchini Syria hazikutafautiana na hatua zake katika vita vya Kujihami Kutakatifu vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Iraq wakati huo dhidi ya Iran. Akaongezea kwa kusema, Shahidi Soleimani na makamanda wengine watajika wa SEPAH akiwemo Shahidi Hamedani walijitolea kwa kila hali na walikuwa wakiichukulia kadhia ya Syria kama jukumu na wajibu mtakatifu.

342/
Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*