?>

Nchi nne wanachama wa EU zataka fedha za Russia zilizozuiliwa zitumike kuijenga upya Ukraine

Nchi nne wanachama wa EU zataka fedha za Russia zilizozuiliwa zitumike kuijenga upya Ukraine

Nchi nne wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) zinatazamiwa kuwasilisha rasmi katika umoja huo barua ya kutaka mali na fedha za Russia zilizozuiliwa na EU zitumiwe kuijenga upya Ukraine baada ya kumalizika vita.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei, Ukraine ilifanya makadirio ya karibu dola bilioni 600 zinazohitajika kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo; na kwa kuzingatia kuendelea kwa vita, inatazamiwa kuwa kiwango hicho kitaongezeka na kuwa kikubwa zaidi.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, katika barua yao hiyo inayotazamiwa kuwasilishwa leo katika mkutano wa mawaziri wa fedha wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, nchi nne za Lithuania, Slovakia, Estonia na Latvia zimeeleza kwamba, sehemu kubwa ya gharama za kuikarabati na kuijenga upya Ukraine ikiwemo gharama ya fidia kwa waathirika wa mashambulio inapasa igharamiwe na Russia.

Barua hiyo aidha imeutaka Umoja wa Ulaya ujiandae kutekeleza vikwazo vingine vipya dhidi ya Moscow.

Hapo awali iliripotiwa kuwa, hadi sasa Umoja wa Ulaya umeshazuia karibu yuro bilioni 30 katika mali za wawekezaji pamoja na taasisi za Russia na Belarus.

Wakati huohuo Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesema, analitambua kuwa ni wizi pendekezo lililotolewa na Mkuu wa Sera za Nje wa EU Josep Borrell la kuzuiliwa akiba ya fedha za kigeni za Russia na kupatiwa Ukraine kwa ajili ya kusaidia gharama za kuijenga upya nchi hiyo.../  


342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*