?>

Nchi za Afrika Mashariki kutuma askari DRC kukabiliana na waasi

Nchi za Afrika Mashariki kutuma askari DRC kukabiliana na waasi

Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitatuma kikosi maalum cha kikanda katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kukabiliana na makundi kadhaa ya watu wenye silaha hasa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Taarifa iliyotolewa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Juni 15 katika nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), alitangaza kuanzishwa kwa Jeshi la Kanda ya Afrika Mashariki chini ya mwamvuli wa EAC kwa lengo kuingilia mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC na kuutatua.

Taarifa hiyo imesema mkutano wa makamanda wa nchi wanachama watakutana Jumapili Juni 19, Nairobi ili kukamilisha maandalizi ya kutumwa kwa Jeshi la Kikanda nchini DRC.

Hali kadhalika taarifa hiyo imesema kikosi cha kikanda kitatumwa katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mara moja ili kuleta utulivu katika eneo hilo na kutekeleza amani na kuunga mkono vikosi vya usalama vya DRC na ushirikiano wa karibu na Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani DRC ambacho ni maarufu kama MONUSCO.

Haya yanajiri kufuatia uasi wa hivi karibuni wa waasi wa M23 ambao serikali ya DRC inadai wanaungwa mkono na nchini jirani ya Rwanda. Hata hivyo Rwanda imekanusha vikali tuhuma hizo.

Katika taarifa yake, Rais Kenyatta aliamuru pia kusitishwa mara moja kwa mapigano Mashariki mwa DRC na makundi yote yenye silaha kuweka silaha chini bila masharti.

Bado haijabainika ni nchi gani zitakazounda kikosi hicho cha kijeshi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki na iwapo Rwanda itakuwa katika kikosi hicho au la.

Rwanda na Uganda ziliivamia DRC mara mbili katika muongo wa tisini na kupelekea kuibuka vita ambavyo vilijumuisha nchi kadhaa na kupelekea mamilioni kuuawa. Vita hivyo viliibua makundi ya waasi ambao bado wanaendeleza harakati zao mashariki mwa DRC.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*