?>

Ombi jipya la Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya

Ombi jipya la Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya

Licha ya kuwepo mivutano mikubwa kati ya viongozi wa Ankara na wa Umoja wa Ulaya katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, lakini serikali ya Uturuki inasema kuwa bado ina nia ya kujiunga na umoja huo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kufuatia maombi ya mara kwa mara ya Uturuki kwa Umoja wa Ulaya, Rais Recep Tayyip Erdogan wa nchi hiyo ameuomba umoja huo ukubali uanachama wa nchi yake baada ya Uingereza kujitoa katika umoja huo, na kuongeza kuwa hakuna wakati ambao Uturuki imefutilia mbali nia yake ya kuutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Matamshi hayo ya rais wa Uturuki yanathibitisha wazi kuwa licha ya kuwepo mivutano na vita vya maneno kati ya viongozi wa serikali ya nchi hiyo na wa Umoja wa Ulaya, lakini Ankara haijavichukulia vita hivyo kuwa mgogoro mkubwa, bali inavitazama kama mbinu ya kudhamini maslahi ya taifa la Uturuki.

Hakuna shaka kwamba harakati za Uturuki katika Bahari ya Mediterania na mvutano wa nchi hiyo na Ugiriki ni mambo ambayo yameandaa uwanja wa kuongezeka hitilafu baina ya Ankara na Brussels.

Wakati huo huo tunapasa kusema kuwa mivutano ambayo imedhihiri kati ya pande mbili hizo katika miezi ya karibuni, imetokana na harakati za Uturuki za kuchimba visima vya mafuta na gesi katika bahari hiyo.

Katika upande wa pili, Ugiriki ikishirikiana na baadhi ya nchi za Ulaya, imezitaja shughuli hizo za Uturuki kuwa zilizo kinyume cha sheria na kuionya Ankara kuhusu suala hilo. Pamoja na hayo Uturuki imepuuzilia mbali onyo hilo na kusisitiza kuwa inaendesha shughuli hizo kwa ajili ya kudhamini haki na maslahi yake mashariki mwa Bahari ya Mediterania na katika maji ya Bahari Nyeusi na ya Aegean.

Hii ni katika hali ambayo shiriki la kijeshi la nchi za Magharibi Nato lilisema siku chache zilizopita kwamba Ugiriki na Uturuki tayari zimeanzisha mawasiliano kwa ajili ya kumaliza mivutano baina yao na kuepusha mapigano katika Bahari ya Mediterania.

Kwa kifupi ni kuwa, uhusiano wa Uturuki na Umoja wa Ulaya katika muongo mmoja uliopita umekuwa wa mivutano na hitilafu nyingi.

Baadhi ya wajuzi wa mambo wanasema kuwa mivutano katika uhusiano wa Uturuki na nchi za Magharibi unatokana na mabadiliko ya mara kwa mara na ya lazima katika siasa za nje za Ankara, jambo ambalo wanasema limewawezesha viongozi wa nchi hiyo kufanikisha siasa zao katika ngazi za kimataifa.

Rais Erdogan kwa muda mrefu amekuwa akiamini kwamba hatimaye Uturuki itajiunga na Umoja wa Ulaya. Akizungumza hivi karibuni na Charles Michel, Mkuu wa Baraza la Ulaya, Rais Erdogan amesema: Kila hatua inayochukuliwa kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa Uturuki na Umoja wa Ulaya, ni fursa mpya kwa maslahi ya pande zote mbili na Ankara inaona kuwa itakuwa pembeni ya umoja huo katika siku zijazo.

Licha ya matamshi hayo ya kutia matumaini lakini baadhi ya wanasiasa wanasema kuwa siasa za serikali ya Ankara za kuibua migogoro ya mara kwa mara na Umoja wa Ulaya bila shaka zinahatarisha maslahi ya taifa la Uturuki yenye jamii ya watu milioni 80. Licha ya matamshi hayo chanya ya viongozi wa Uturuki kuhusiana na uhusano wao na Umoja wa Ulaya lakini ni wazi kuwa nchi hiyo haitapewa uanachama katika umoja huo katika miaka miaka michache ijayo.

Uturuki iliwasilisha rasmi ombi lake la kujiunga na Umoja wa Ulaya tarehe 14 Aprili 1987, lakini ombi lake hilo likatambuliwa rasmi na umoja huo tarehe 12 Disemba 1999, ambapo mazungumzo ya nchi hiyo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya yalianza tarehe 3 Oktoba 2005.

Licha ya kuwa mazungumzo ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya yalianza tarehe iliyotajwa lakini kungali kuna vizingiti na vikwazo vikubwa katika njia ya nchi hiyo kupewa uanachama katika Umoja wa Ulaya, zikiwemo hitilafu za kisiasa na masuala ya ardhi na Cyprus na vilevile hitilafu za kisiasa na Ugiriki, nchi mbili ambazo zote ni wanachama kamili wa umoja huo.

342/
Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*