?>

Rais Samia Suluhu na Obasanjo wajadili hali ya usalama barani Afrika

Rais Samia Suluhu na Obasanjo wajadili hali ya usalama barani Afrika

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo na kujadili changamoto mbalimbali likiwemo suala la usalama barani Afrika.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma ambapo wawili hao wamezungumzia umuhimu wa wakuu wa nchi kujadiliana na kutafuta suluhisho la migogoro mbalimbali inayozikabili nchi zao ambayo inasababisha vifo vya watu wasio na hatia hasa wanawake na watoto wadogo.

Aidha Rais Samia na Rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjano wamezungumzia masuala ya maendeleo hasa katika uchumi na kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuongeza ushirikiano na kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji ili kurahisha mambo katika sekta ya biashara.

Rais Mstaafu wa Nigeria Obasanjo ametoa pia salamu zake za rambirambi kwa Rais Samia kufuatia vifo vya waliokuwa Marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Hayati Benjamin William Mkapa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli waliofariki dunia tarehe 23 Julai, 2020 na tarehe 17 Machi, 2021 mtawalia.

Rais Mstaafu Obasanjo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupokea kijiti cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amemtakia kila la heri katika majukumu yake.

Samia Suluhu Hassan ambaye ameandika historia ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na Afrika Mashariki, ndiye Rais wa kwanza mwanamke Mwislamu barani Afrika anayejistiri na kuvaa vazi la hijabu.

Mama Samia alichukua hatamu za uongozi kama rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi mwaka huu baada ya kuaga dunia aliyekuwa Rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*