?>

Russia yasambaratisha kwa makombora maghala mengine ya silaha za Ukraine

Russia yasambaratisha kwa makombora maghala mengine ya silaha za Ukraine

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi wa Russia amesema kuwa ndege za kivita za nchi hiyo zimesambaratisha kwa makombora maghala mengine ya silaha za Ukraine.

Shirika la habari la TASS limemnukuu Jenerali Igor Konashenkov akitangaza habari hiyo jana na kuongeza kuwa, miongoni mwa silaha za Ukraine zilizoteketezwa kwenye mashambulizi hayo ya ndege za Russia ni mabomu ya vishada na zana nyingine za kijeshi.

Amesema, mashambulio hayo ya anga yamesambaratisha maghala ya silaha ya maeneo ya Lysychansk, Kharkiv na kadhalika.

Kabla ya hapo, Rais Vladimir Putin wa Russia naye alikuwa ameonya kuwa Moscow itakuwa inashambulia silaha zozote za Ukraine hususan zile ambazo nchi za Magharibi zinaipa nchi hiyo na kusisitiza pia kwamba, mgogoro wa chakula duniani hausababishwi na Russia, bali ni nchi za Magharibi ndizo zinazoiamulia Ukraine nini cha kufanya na ndizo zinazozuia bidhaa zisitoke nchini humo.

Rais huyo wa Russia amesema, ukoloni mamboleo ndio unaosababisha migogoro wa kibinadamu katika sehemu mbalimbali duniani; na kwamba Marekani na nchi za Ulaya ndizo zinazopaswa kubebeshwa dhima la matatizo hayo.

Putin alisema hayo katika hotuba yake muhimu ya siku ya Ijumaa na kuongeza kuwa, usimamizi mbaya wa Wamagharibi kwa uchumi wa dunia na kuyanyonya mataifa dhaifu ndiyo sababu kuu ya kushuhudiwa mfumko wa bei za bidhaa na mgogoro wa chakula duniani hivi sasa.

Rais wa Russia alisisitiza pia kuwa, "ongezeko la bei ya mafuta duniani, mfumko wa bei za bidhaa, migogoro ya chakula, gesi na mafuta yote hayo yametokana na makosa ya kimfumo kwenye sera ya uchumi ya utawala wa sasa wa Marekani, na madola ya Ulaya."

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*