?>

Sababu za maandamano ya Wapalestina wa Ramallah dhidi ya Serikali ya Mamlaka ya Ndani

Sababu za maandamano ya Wapalestina wa Ramallah dhidi ya Serikali ya Mamlaka ya Ndani

Wananchi wa Palestina wamefanya maandamano ya upinzani katika mji wa Ramallah, Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan wakitaka kuvunjwa Serikali ya Mamlaka ya Ndani na kung'atuka madarakani rais wake Mahmoud Abbas.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Tangu mwaka 1994, wakati Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilipoundwa kwa mujibu wa mkataba wa Oslo, haya ni maandamano ya pili makubwa ya umma kufanyika katika Ufukwe wa Magharibi dhidi ya Mamlaka hiyo. Maandamano ya kwanza yalifanyika mwaka 2012, ambapo Wapalestina wa eneo hilo la ardhi za Palestina walifanya maandamano dhidi ya serikali hiyo ya Mahmoud Abbas. Katika maandamano hayo, takwa kuu la wananchi lilikuwa ni kudhibitiwa ughali wa bidhaa za mahitaji ya msingi hususan nishati na fueli za vyombo vya usafiri. Joto la maandamano ya 2012 lilipoa baada ya kipindi cha miezi sita kufuatia kuchukuliwa hatua za kudhibiti bei za baadhi ya bidhaa hizo.

Maandamano ya sasa, kama tulivyotangulia kueleza, ni ya pili ya upinzani dhidi ya Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Tofauti ya maandamano haya na yale ya mwaka 2012 ni kwamba, maandamano ya 2012 yalizimika na kupoa kirahisi kwa kudhibitiwa bei za bidhaa tu, lakini katika maandamano yao ya sasa Wapalestina wa Ufukwe wa Magharibi wanatoa nara na kaulimbiu dhidi ya Abu Mazin na serikali anayoongoza na kwa mara ya kwanza wanapaza sauti kutaka serikali hiyo ivunjwe. Kuna sababu kadhaa za msingi zilizochochea maandamano ya sasa dhidi ya Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Kwanza ni kwamba, wananchi wa Palestina hawaridhishwi na mkakati wa kufanya mazungumzo ya mapatano unaotekelezwa na Serikali ya Mamlaka ya Ndani na wala hawaamini kama utaweza kudhamini maslahi yao. Katika miezi ya karibuni, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umeendesha kampeni ya ukatili na ukandamizaji dhidi ya Wapalestina wa Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu na Ufukwe wa Magharibi, ambao ndio uliopelekea pia kuzuka vita vya siku 12 mnamo mwezi Mei.

Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina haikuchukua hatua yoyote ya maana kukabiliana na jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Quds na Ufukwe wa Magharibi zaidi ya kuziandikia barua tu baadhi ya taasisi za kimataifa. Wakati wa vita hivyo vya siku 12, serikali ya Mahmoud Abbas si tu haikuyasaidia wala kuyaunga mkono makundi ya muqawama ya Palestina ya Ukanda wa Gaza, lakini iliamua pia kuendelea kufanya hata mazungumzo ya siri na mashirikiano ya kiusalama na Israel.

Sababu nyingine iliyochochea maandamano dhidi ya Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika Ufukwe wa Magharibi ni ukatili na ukandamizaji mkubwa unaofanywa na mamlaka hiyo katika kukabiliana na wapinzani na wakosoaji wake. Kilele cha ukatili huo ni ule aliofanyiwa Nazar Banat, mkosoaji wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ambao ulipelekea mwanaharakati huyo kufa shahidi. Kosa la Nazar Banat lilikuwa ni kuikosoa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na mwito aliotoa kwa Umoja wa Ulaya wa kuutaka ukate misaada yake kwa mamlaka hiyo kwa sababu ya kuchelewesha kuitisha uchaguzi wa rais na bunge la Palestina.

Baada ya kufa shahidi Nazar Banat, Wapalestina wa Ramallah walikusanyika na kufanya mgomo wa kuketi kwenye uwanja wa mzunguko wa Al Manarah wakitaka maafisa waliohusika na jinai ya kumuua mwanaharakati huyo wachukuliwe hatua; na serikali na makamanda wa vyombo vya usalama vya Mamlaka hiyo ya Ndani ya Palestina wajiuzulu. Askari wa usalama wa Mamlaka ya Ndani waliovalia kiraia waliwashambulia waaandamanaji katika mji wa Ramallah na kuwajeruhi kadhaa miongoni mwao. Muamala huo wa kikatili umechangia kuendelea maandamano ya upinzani dhidi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na wananchi kutaka rais wa mamlaka hiyo Mahmoud Abbas ang'atuke madarakani; kwa sababu waandamanaji hao wanaitakidi kuwa Abbas ameshapoteza uhalali wake wa kisiasa.

Sababu nyingine iliyochangia kuendelea maandamano dhidi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ni kucheleweshwa uchaguzi wa bunge na wa rais wa Mamlaka hiyo. Baada ya kupita miaka 15, uchaguzi wa bunge la Palestina ulikuwa umepangwa ufanyike tarehe 22 Mei mwaka huu, wa rais wa Mamlaka ya Ndani tarehe 31 Julai na ule wa Baraza la Taifa la Palestina tarehe 31 Agosti. Baada ya kubainika kuwa harakati ya Hamas ilikuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa bunge, kwa kutumia kisingizio kwamba Israel hairuhusu uchaguzi huo ufanyike pia katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, Mahmoud Abbas aliakhirisha uchaguzi huo wa bunge; na kwa msingi huo ikaamuliwa chaguzi zingine mbili pia zisifanyike. Hatua hiyo imechangia sana kufanyika maandamano dhidi ya mamlaka ya ndani na hasa rais wake Abbas. Wananchi wa Palestina wanaitakidi kuwa kwa kucheleweshwa chaguzi hizo hakutakuwa na muelekeo wa wazi wa kisiasa huko Palestina na hivyo kuendelezwa mwenendo wa kukwamisha mchakato wa uchaguzi, unaoshuhudiwa kwa mwaka wa 15 sasa.../

342/

Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*