?>

Siku ya huzuni kwa Mashia duniani

Siku ya huzuni kwa Mashia duniani

Siku kama hii ya leo ni siku ulimwengu uliondokewa na mwanazuni muhimu katika historia ya kiislamu nae Imam Jaafar Saadiq(as) mwalimu mwenye taathira kubwa katika kuendeleza harakati za uislamu.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Siku hii ni siku ambayo Waislamu lazima kuikumubka kwa kuondoka mwalimu na wa maimamu ya Madhehebu mane.

Imam Jaafar Saadiq(as) ni Imam maarufu katika pande zote mbili za Mashia na Masunni na alikuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza Uislamu.

Imam Jaafar Sadiq (AS) alizaliwa mwezi 17 Mfunguo Sita, Rabiul Awwal mwaka 83 Hijria katika mji mtukufu wa Madina. Baba yake ni Imam Muhammad Baqir (AS). Zama za Imam Saidq (AS) zilikuwa moja ya zama za matukio mengi zaidi katika historia ya Uislamu, kwa sababu zilisadifiana na kipindi cha kuondoka hatamu za utawala kutoka mikononi mwa Bani Umayyah na kuingia mikononi mwa Bani Abbas.

Kwa upande mwengine zama hizo zilikuwa za mpambano baina ya nadharia, itikadi na idiolojia mbalimbali na mchuano wa fikra katika Falsafa na Ilmul kalam. Nao Waislamu wa wakati huo walionyesha kuwa na shauku na hamu kubwa ya kujifunza na kuzielewa elimu mbalimbali.

Katika hali kama hiyo bila shaka kuyumba na kuzembea maulamaa wa dini kungesababisha watu kupotoka na kuwa na ufahamu potofu juu ya Uislamu. Katika kipindi hicho nyeti, na kutokana na kuyaelewa mahitaji ya zama, Imam Jaafar Sadiq (AS) alifanya hima kubwa ya kuhuisha na kueneza mafundisho asili ya Uislamu na akaasisi chuo na madrasa ambayo matunda yake yalikuwa ni kupatikana wanafunzi elfu nne waliohitimu na kubobea kwenye fani mbalimbali za elimu.

Katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni tutadondoa baadhi ya johari za dafina ya elimu ya mtukufu huyo zinazohusu miongozo yake juu ya Kitabu cha Wahyi, yaani Qur'ani Tukufu.

Kama mjuavyo wapenzi wasikilizaji moja ya masuali yanayoulizwa kila mara kuhusu Qur'ani ni je kitabu hicho cha mbinguni kimekusanya ndani yake elimu zote wanazohitajia wanadamu? Kutokana na dhahiri ya aya za Qur'ani Tukufu inafahamika kuwa kitabu hicho kimebainisha "kila kitu". Allamah Tabatabai, mfasiri mkubwa wa Qur'ani anasema: "Madhumuni ya "kila kitu" ni masuala yanayohusiana na uongofu wa mwanadamu; yaani mafundisho sahihi na halisi kuhusu ulimwengu, chanzo cha kila kitu, ufufuo, akhlaqi njema, sheria za dini, visa na mawaidha." Imenukuliwa kutoka kwa Imam Sadiq (AS) kwamba amesema:"Mwenyezi Mungu Mtukufu na Aliyetukuka amebainisha kila kitu ndani ya Qur'ani. Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hajakipunguza kitu, kati ya chochote wanachohitajia watu, ila jambo hilo litakuwa limeteremshwa ndani ya Qur'ani ili asije akatokea mtu akasema, kama jambo fulani lingekuwa sahihi lingeteremshwa katika Qur'ani."

Aidha mtukufu huyo amenukuliwa akisema: "Hakuna jambo lolote ambalo watu wawili watakuwa wanahitilafiana juu yake ila asili ya utatuzi wake utakuwa umo ndani ya Qur'ani, lakini akili za watu zinashindwa kulidiriki." Kutokana na hadithi hii tunaweza kusema kuwa kila kitu kimebainishwa ndani ya Qur'ani, lakini uwezo wa kuyafahamu mambo yote hayo uko nje ya uwezo wa ufahamu wa mwanadamu asiye maasumu. Kuhusiana na jambo hilo Imam Jaafar Sadiq (AS) amesema:"Mimi ninakifahamu Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ndani yake umeelezewa mwanzo wa uumbaji na yale yatakayojiri mpaka Siku ya Kiyama. Ndani yake zimo habari za mbinguni na ardhini, habari za Pepo na Jahanamu na habari za yaliyopita na ya sasa; na mimi ninayajua hayo kama ninavyokiangalia kiganja cha mkono wangu".

Watu walimuuliza Imam Jaafar Sadiq, "Ni vipi kwamba licha ya kupita zama, Qur'ani ingali na upya uleule?" Imam akawajibu kwa kusema:" Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliyetukuka hakuifanya Qur'ani iwe ni kwa ajili ya zama makhsusi na kwa watu makhsusi. Kwa sababu hiyo Qur'ani ni mpya katika kila zama na kwa kila kaumu ya watu mpaka Siku ya Kiyama".

Madhumuni ya Imam Sadiq ni kwamba Mwenyezi Mungu ameiteremsha Qur'ani kwa namna ambayo inawiyana na kila zama na inakidhi mahitaji ya wanadamu wote; kwa sababu kutokana na kubainisha kaida na kanuni jumla na kutokana na kuwepo Uimamu kando yake na kuendelea kwa ijtihadi, Qur'ani inao uwezo wa kuyakidhi na kuyapatia jibu mahitaji ya kila zama na mahala kutokana na kuweza kutoa yaliyomo ndani yake na kuyatabikisha na misdaqi na mifano hai mipya."

Kuifahamu Qur'ani, ambacho ni kitabu cha mbinguni kilichokamilika zaidi ni jambo la lazima. Imam Jaafar Sadiq (AS) amesema kuhusu jambo hilo kuwa:"Inavyostahiki kwa muumini ni kwamba asife ila awe ameshajitaalamisha Qur'ani au awe yumo katika hali ya kujitaalamisha".

Katika maneno haya, makusudio ya kujitaalamisha na kujifunza si kwa maana ya kuweza kuisoma tu bali ni kujifunza kwa kuelewa maana ya Qur'ani na kuyafahamu maamrisho yaliyomo ndani yake na hatimaye kukifuata kivitendo kitabu hicho. Ushahidi wa haya ni maelezo ya ufafanuzi aliyoyatoa yeye mwenyewe Imam Jaafar Sadiq kuhusu watu wanaoisoma Qur'ani kwa namna inayostahiki. Imam amesema: "Watu wa aina hiyo wanazisoma aya za Qur'ani kwa usomaji sahihi, wanazifahamu maana yake na wanazitekeleza hukumu zake; wanapata matumaini kutokana na ahadi zake na wanazihofu adhabu zake, wanazingatia visa vyake na kupata ibra kutokana na mifano yake; wanatekeleza maamrisho yake na wanajiweka mbali na makatazo yake. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba usomaji si wa kuhifadhi aya za Qur'ani tu na kubainisha herufi na kusoma sura zake…watu wamezihifadhi herufi za Qur'ani, wakazisoma kwa namna ya kuvutia lakini wakaikengeuka mipaka yake; hivyo lengo la kusoma ni kutadabari katika aya za Qur'ani.

Kuna mtu alimuuliza Imam Jaafar Sadiq (AS): Nini makusudio ya aya hii ya 59 ya Suratun Nisaa ambayo Mwenyezi Mungu anasema mtiini Mwenyezi Mungu, Mtume na Ulul amr? Ulul amr ni watu gani? Imam Sadiq akasema:"Mwenyezi Mungu ametukusudia sisi tu Ahlul Bayt na amewaamrisha waumini watutii sisi mpaka Siku ya Kiyama." Akaulizwa Imam:" Mbona jina la Ali na Ahlul Bayt halikutajwa ndani ya Qur'ani?" Mtukufu huyo akajibu kwa kusema:" Mwenyezi Mungu ameamrisha Sala ndani ya Qur'ani lakini hakusema iwe ni rakaa tatu au nne; mpaka Mtume alipotoa tafsiri (kwa kubainisha idadi ya rakaa); na aya ya Zaka ilishuka lakini Mtume ndiye aliyeifasiri, na kuhusu Hija ilishuka aya lakini haikusema fanyeni amali ya kutufu Nyumba (ya Al Kaaba) mara saba; mpaka pale Mtume wa Allah alipoitafsiri. 

Hivyo na aya ya "Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi.. nayo pia iliteremshwa kumhusu Ali, Hassan na Hussein ( lakini majina yao hayakutajwa). Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema kumhusu Ali:" Kila yule ambaye mimi namtawalia mambo yake, Ali pia anamtawalia mambo yake", na akasema:"Ninakuusieni juu ya Qur'ani na Ahlul Bayt wangu; kwa sababu mimi nimemwomba Mwenyezi Mungu viwili hivyo visitenganike mpaka vitapoingia pamoja nami kwenye hodhi la (Kauthar). Na Mwenyezi Mungu amenipa hilo. Na kisha Mtume amesema:"Nyinyi msiwafundishe kitu chochote Ahlul Bayt wangu; kwa sababu wao ni wajuzi zaidi kuliko nyinyi. Wao hawakutoeni nyinyi nje ya njia ya uongofu na wala hawakuingizeni kwenye upotofu".

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*