?>

Sisitizo la viongozi wa Korea Kaskazini kuhusu kuimarisha uwezo wa kijeshi

Sisitizo la viongozi wa Korea Kaskazini kuhusu kuimarisha uwezo wa kijeshi

Kiongozi wa Korea Kaskazini ametaka uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo uzidi kuimarishwa. Vyombo vya habari vya Pyongyang vimetangaza kuwa, Kim Jong-un Kiongozi wa Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili ameshiriki na kusimamia mazoezi ya makombora ambayo yamefanyika kwa mafanikio.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Baada ya kusimamia zoezi la majaribio ya makombora hayo mapya, Kiongozi wa Korea Kaskazini amesisitiza ulazima wa kuimarishwa nguvu za kimkakati za kijeshi nchini humo.

Majaribio hayo ya makombora ya hivi karibuni yalikuwa ya kwanza rasmi baada ya yale yaliyofanyika Machi 2020.

Katika majaribio hayo ya makombora mapya ya Korea Kaskazini kulifanyika jaribio la kombora lenye mwendo wa kasi mara kadhaa kuliko kasi ya sauti (hypersonic) ambalo limefanikiwa kulenga shabaha kwa ustadi mkubwa baada ya kusafiri umbali wa kilomita 1000.

Sisitizo la Kiongozi wa Korea Kaskazini kuhusu kuimarishwa uwezo wa kijeshi wa nchi hiyo ni katika fremu ya mkakati ambao Pyongyang imekuwa ikiufuatilia katika miaka ya hivi karibuni kufuatia taharuki za kijeshi za Marekani katika Rasi ya Korea ambapo imekuwa ikifanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja na Korea Kusini.

Katika miaka ya hivi karibuni, mbali na kuwa Marekani imekuwa ikiibua mazingira ya kipropaganda yenye lengo la kuvuruga usalama wa Korea Kaskazini kwa kuweka mfumo wa makombora wa THAAD  sambamba na kufanya mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini, pia inaendelea kutoa vitisho vya kuivamia kijeshi Korea Kaskazini. Hakuna shaka kuwa taharuki hizo za Marekani zimeilazimu Korea Kaskazini kuwa na azma ya kuimarisha uwezo wake wa kijeshi ili iweze kumzuia adui endapo atathubutu kuivamia nchi hiyo.

Katika duru ya kwanza ya urais wa Donald Trump, kulishuhudiwa uhasama mkubwa katika uhusiano wa Korea Kaskazini na Marekani na jambo hilo lilipelekea nchi hizo mbili kuanza mazungumzo ya kupunguza uhasama baina yao.

Duru ya kwanza ya mazungumzo baina ya Kim Jong-un na Donald Trump ilifanyika Juni 2018 kwa uwenyeji wa Singapore ambapo katika kikao hicho Marekani iliahidi kuanza kuondoa makombora yake ya nyuklia katika Rasi ya Korea sambamba na kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini ilitekeleza ahadi yake ya kusitisha majaribio ya makombora na silaha za nyuklia. Licha ya hatua hizo chanya za Korea Kaskazini, si tu kuwa Marekani haikuondoa vikwazo dhidi ya nchi hiyo bali ilichukua hatua za kichochezi dhidi ya Pyongyang katika Rasi ya Korea.

Pamoja na kuwa  Marekani ilikuwa haijaondoa vikwazo kama ilivyoahidi, Kionozi wa Korea Kaskazini alishiriki katika duru ya pili ya mazungumzo na Trump iliyofanyika Februari 2019. Katika kikao hicho rais huyo wa Marekani alidai kuwa angeisaidia Kora Kaskazini iwe nchi yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi.

Baada ya duru hiyo ya pili ya mazungumzo na kufuatia Marekani kukiuka ahadi zake, Korea Kaskazini ilianza tena majaribio ya nyuklia na makombora na ikasema itasitisha hatua zake hizo kwa sharti la Marekani kurejea katika utekelezaji ahadi zake kikamilifu.

Kufuatia kuingia madarakani Joe Biden kama rais wa Marekani, faili la Korea Kaskazini linaonekana kutokuwa katika kipaumbele cha Ikulu ya White House. Lakini pamoja na hayo Marekani ingali inaendeleza sera za uhasama dhidi ya Korea Kaskaini na jambo hilo limewafanya wakuu wa Pyongyang kuamua kusonga mbele na mkakati wao wa kujiimarisha kijeshi ili kukabiliana na vitio vya Washington.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*