?>

Trump; maafa na msiba kwa haki za binadamu

Trump; maafa na msiba kwa haki za binadamu

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake wenye utata mwingi nchini Marekani, Rais Donald Trump ameacha nyuma historia nyeusi kuhusu suala zima la haki za binadamu, huku akilaumiwa na kukosolewa vikali katika siku za mwisho za utawala wake.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kenneth Roth, mkurugenzi mtendaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lenye makao yake nchini Marekani amesema katika ripoti ya kila mwaka ya shirika hilo kwamba Trump amekuwa msiba mkubwa kwa haki za binadamu na kusisitiza kuwa katika miaka minne ya uongoza wake hakujali kabisa na hata kuchukua misimamo ya uadui na chuki dhidi ya masuala ya haki za binadamu. Amesema, amepuuza haki za binadamu nchini kwake, kuchochea ukiukaji wa haki za binadamu nje ya mipaka ya Marekani na hivyo kudhoofisha pakubwa itibari ya nchi hiyo ulimwenguni.

Katika miaka minne ya utawala wake, Trump amefanya juhudi kubwa za kuongeza na kuchochea misimamo ya ubaguzi wa rangi ndani ya nchi hiyo na kutokana na misimamo yake ghalati katika uwanja huo, ameyashajiisha makundi ya ubaguzi wa rangi na yanayojiona kuwa bora kuliko jamii nyingine, kutekeleza vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi ya jamii hizo.

Kwa mujibu wa Luis Gutiérrez, mbunge wa zamani wa chama cha Democrat katika Congress ya Marekani, sasa imebainika wazi kwamba Trump ni mbaguzi wa rangi moja kwa moja na hakubaliani na thamani ambazo zinadhaminiwa na katiba yetu.

Katika upande mwingine, jamii za waliowachache zimekabiliwa na mashinikizo makubwa ya ubaguzi wa rangi katika utawala wa Trump, kuliko utawala wa rais mwingine yeyote wa Marekani. Mfano wa wazi katika uwanja huo ni kushinikizwa na kufukuzwa nchini Marekani wahajiri wa nchi za Amerika ya Latini na wakati huo huo kuzuiwa raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu kukanyaga ardhi ya Marekani.

Mfano wa wazi zaidi wa kukanyagwa haki za binadamu nchini Marekani katika utawala wa Trump ni kuongezeka vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi ya jamii ya Wamarekani wenye adili ya Afrika na hasa kutoka kwa polisi ya nchi hiyo. Mfano wa wazi zaidi ni radiamali iliyotolewa na Trump kufuatia mauaji ya kinyama yaliyotekelezwa na polisi dhidi ya raia mweusi wa nchi hiyo kwa jila la George Floyd mnamo tarehe 25 Mei katika mji wa Minneapolis katika jimbo la Minnesota, kitendo kilichoamsha hasira na malalamiko makubwa ambayo yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa tena katika miji mingi ya nchi hiyo, kwa ajili ya kulalamikia unyama huo uliotokana na kukita mizizi ubaguzi wa rangi katika jamii ya Marekani.

Badala ya kuomboleza na familia ya muhanga na kukabiliana na wahalifu waliohusika na mauaji hayo ya kinyama, Trump alitoa amri ya kukandamizwa walalamikaji na hata kuamuru jeshi la taifa lipelekwe katika baadhi ya miji iliyoshuhudia malalamiko makubwa zaidi kwa ajili ya kuvunja maandamano ya watu waliomiminika mitaani kulaani mauaji hayo.

Mfano mwingine wa wazi wa ukiukaji wa Trump dhidi ya haki za binadamu, ni dhulma yake ya wazi dhidi ya baadhi ya nchi zinazopinga ubeberu duniani zikiwemo Iran, Venezuela na Cuba. Katika kipindi cha utawala wake, Trump aliziwekea nchi hizo vikwazo vikali na vya kulemaza na hivyo kuwadhuru moja kwa moja raia wa nchi hizo. Kichekesho ni kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imekuwa ikizutuhumu nchi hizo kuwa zinakiuka haki za binadamu. Hii ni katika hali ambayo nchi hiyo hiyo ya kibeberu ya Magharibi imekuwa ikipuuza na kufumbia macho ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na washirika wake wa eneo kama vile Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel. Kwa mujibu wa Kenneth Roth, mkurugenzi mtendaji wa Human Rights Watch, madai hayo ya Marekani dhidi ya Venezuela, Cuba na  Iran yalipoteza maana pale Washington ilipochukua hatua ya kutetea na kusifu rekodi ya Saudi Arabia na utawala wa Israel katika uwanja huo.

Utawala wa Isreal umekuwa ukitekeleza jinai za kutisha dhidi ya watu wa Palestina. Saudi Arabia nayo ina rekodi na historia nyeusi katika uwanja wa haki za binadamu, mfano wa wazi kuhusu hilo ikiwa ni mauaji ya kutisha na kinyama yaliyotekelezwa dhidi ya mwandishi mkosoaji wa utawala wa Riyadh Kamal Khashoggi, aliyeuawa kwa amri ya moja kwa moja ya Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo. Katika uwanja huo pia, Trump alifumbia macho suala zima la haki za binadamu na kutochukua hatua yoyote ya kumuadhibu Bin Salman, kutokana na maslahi yake ya kiuchumi na kibiashara na nchi hiyo ya kifalme.

342/Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*