?>

Uganda kuteketeza dozi laki nne (400,000) za chanjo za UVIKO-19

Uganda kuteketeza dozi laki nne (400,000) za chanjo za UVIKO-19

Serikali ya Uganda ina mpango wa kuteketeza dozi laki nne za chanjo za UVIKO-19 au corona baada ya chanjo hizo kuharibika kutokana na utunzaji mbaya katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Waziri wa Afya wa Uganda, Dk Jane Ruth Aceng ametangaza habari hiyo na kusema kuwa, chanjo hizo zilipelekwa kwenye mikoa ya kaskazini mwa Uganda lakini hazikutumika.

Amesema, sehemu kubwa ya chanjo zilizoharibika ni za Moderna na AstraZeneca na ndizo ambazo zitateketezwa ili kuondoa kabisa uwezekano wa kutumiwa.

Waziri wa Afya wa Uganda, Bi Aceng yuko mstari wa mbele kuwashajiisha na kuwahamasisha wananchi wa nchi hiyo wapige chanjo za ugonjwa wa UVIKO-19 au corona.

Serikali ya Uganda imesema ni lazima kwa wafanyakazi wa serikali wakiwemo walimu kupiga chanjo za corona na si jambo la hiari kwao.

Lengo la msimamo huo wa serikali ya Kampala ni kuhakikisha ugonjwa wa corona unatokomezwa na nchi inakuwa salama, na hilo halitowezekana isipokuwa kwa kupigwa chanjo idadi kubwa ya watu hasa wenye maingiliano na watu wengi kama walimu, wahudumu wa afya, watu wa usafiri na watu wa masokoni. 

Hadi wakati tunaandika habari hii, idadi ya wagonjwa wa corona waliothibitishwa na kutangazwa na serikali ya Uganda ilikuwa ni 156,637 na waliofariki dunia hadi wakati huo walikuwa ni wagonjwa 3,378 katika kona mbalimbali za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Uganda imeshapiga chanjo milioni 12, na laki mbili na 20,106 (12,220,106 ) za corona zilizotengenezwa na mashirika ya nchi mbalimbali duniani.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*