?>

Ujumbe wa Hija wa Kiongozi wa Mapinduzi kwa Waislamu Duniani; sisitizo la mapambano dhidi ya madola ya kichokozi na hasa Marekani.

Ujumbe wa Hija wa Kiongozi wa Mapinduzi kwa Waislamu Duniani; sisitizo la mapambano dhidi ya madola ya kichokozi na hasa Marekani.

Katika ujumbe wake wa Hija kwa Waislamu duniani, Ayatullah Ali Khamanei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuendelea kuhuzunika nyoyo za Wailsmu walio na hamu kubwa ya kwenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba, kutokana na janga la corona na kusema kuwa huo ni mtihani wa muda tu ambao utamalizika kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Amesema licha ya kuwepo janga hilo ambalo limewazuia Waislamu wengi kutekeleza ibada ya Hija lakini hilo halipasi kupelekea ujumbe wa ibada hiyo muhimu, likiwemo suala la kupambana na madola yenye kiburi na ya kichokozi na hasa Marekani, kusahaulika.

Ameashiria matatizo na changamoto nyingi zinazoukabili ulimwewngu wa Kiislamu na kusema kuwa licha ya uwepo wa changamoto hizo lakini ushindi wa mrengo wa mapambano na mwamko unaoonekana katika nchi za Kiislamu na hasa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, Yemen, Syria na Iraq ni miongoni mwa mambo yanayotia matumaini. Amesisitiza kwamba: Ahadi ya kweli ya Mwenyezi Mungu ni kuwanusuru Mujahideena na taathira ya kwanza ya juhudi na jitihada hizo ni kunyimwa Marekani na nchi nyingine zinazotumia mabavu, fursa ya kuingilia na kueneza shari katika nchi za Kiislamu.

Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu, Hija ni chimbuko la uwezo na nguvu ya Uslamu kuhusu masuala mengi na hivyo haipaswi kupuuzwa wala kusahaulika katika hali yoyote ile.

Kwa msingi huo ujumbe wa Hija wa Kiongozi Muadhamu una umuhimu mkubwa kwa kuzingatia nukta mbili kuu:

Nukta ya kwanza ni kuwa unasisitiza udharura wa kupambana na kusimama imara mbele ya madola ya kibeberu katika upeo wa kitaifa, kieneo na kimataifa.

Nukta ya pili ni kwamba unabainisha wazi matunda na taathira ya mwamko wa mataifa ya Kiislamu, ambao umeibua mapambano dhidi ya mfumo wa kibeberu ulimwenguni.

Huku akibainisha umuhimu wa suala hilo, Ayatullah Khamenei amesema: Mataifa ya eneo yamethibitisha kwamba yako macho na kuwa yamejitenga na tawala ambazo ziko tayari kuiridhisha Marekani na kukidhi matakwa yake katika kila hali, likiwemo suala nyeti mno la Palestina.

Kutekelezwa ibada halisi ya Hija, kwa kutilia maanani vigezo vyake vya umoja na mshikamano, kuna taathira kubwa kwa mustakbali wa Uma wa Kiislamu na mataifa mengine yote yanayodhulumiwa na tawala za kibeberu. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasisitiza kwamba: Ujumbe muhimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ambao umeutia wasi wasi mkubwa na hasira ulimwengu wa kiistikbari ni wito wake wa mapambano; mapambano dhidi dhidi ya uingiliaji na shari ya Marekani na madola mengine ya kichokozi, na kuzingatia masuala ya mustakbali wa ulimwengu wa Kiislamu kwa msingi wa mafundisho ya Uislamu.

Kama ilivyosisitizwa katika ujumbe wa Kiongozi Muadhamu, ni wazi kuwa Marekai na washirika wake wana wasi wasi mkubwa kuhusiana na suala zima la mapambano na hivyo wameamua kutumia kila mbinu kukabiliana na mrengo wa mapambano hayo.

Kuhusu hilo, Kiongozi Muadhamu amesema kwamba juhudi za kipropaganda zinazofanywa na Marekani kwa ajili ya kupotosha ukweli wa mambo na kuwatuhumu vijana shujaa na jasiri wanaofuatilia matakwa na malengo yao matukufu, kuwa wanatumikia malengo ya Iran na nchi nyingine ni aina fulani ya dharau na udhalilishaji wa vijana hao na kuwa tuhuma hizo zinatokana na Marekani kutotambua wala kuyadiriki vyema mataifa ya eneo hili. Amesema kushindwa huko kwa Wamarekani kuyadiriki mataifa ya eneo ndiko kumewafanya washindwe nchini Afghanistan na hatimaye kulazimika kuondoka kwa madhila katika nchi hiyo baada ya kuingia huko kijeshi kwa mbwembwe na makelele mengi miaka 20 iliyopita. Hata hivyo wamelazika kuondoka kwa madhila katika nchi hiyo baada ya kutekeleza mauaji mengi ya kinyama dhidi ya raia wa kawaida na wasio na hatia.

Uzoefu wa miongo mitatu iliyopita unaonyesha wazi kuwa uwepo wa kijeshi wa Marekani Asia Magharibi umesababisha vita, mauaji ya umati, ghasia na machafuko, uharibifu na kuyabakisha nyuma kimaendeleo mataifa ya eneo, hivyo ni wazi kuwa Marekani inapaswa kuwajibishwa kutokana na matokeo machungu ya uingiliaji wake katika eneo.

Kwa mtazamo huo ujumbe wa Hija wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu una nukta muhimu na za kistratijia ambazo iwapo zitatekelezwa vyema na hasa katika kipindi hiki nyeti bila shaka zinaweza kuwa na taathira kubwa kwa mustakbali wa ulimwengu wa Kiislamu na hasa mataifa ya eneo la Asia Magharibi.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*