?>

Umoja wa Mataifa wazindua mpango mkubwa wa misaada kwa Afghanistan

Umoja wa Mataifa wazindua mpango mkubwa wa misaada kwa Afghanistan

Umoja wa Mataifa na washirika wake hii leo umezindua mpango wa kusaidia watu milioni 28 wenye uhitaji mkubwa wa misaada ya kubinadamu nchini Afghanistan pamoja na nchi nyingine jirani.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Uzinduzi huo ulifanyika mjini Geneva Uswisi Jumatatu ambapo Umoja wa Mataifa na mashirika matano yasiyo ya kiserikali yamelenga kuwasaidia wananchi milioni 22 wa Afghanistan pamoja na wengine milioni 5.7 wanaoishi kama wakimbizi katika nchi tano jirani sambamba na jamii za wazawa zilizowakaribisha.

Majanga ya kibinadamu yanaendelea kuikabili nchi hiyo ambapo taarifa zinaeleza kuwa nusu ya watu wanakabiliwa na njaa kali, zaidi ya watu milioni 9 wamekimbia makazi yao, mamilioni ya watoto hawaendi shule, ukiukwaji wa haki za kimsingi za wanawake na wasichana, wakulima na wafugaji wanataabika huku kukiwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, na uchumi unazidi kudorora. Na kama hayo hayatoshi makumi ya maelfu ya watoto wako katika hatari ya kufa kutokana na utapiamlo huku huduma za kimsingi za afya zikiporomoka.

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA Martin Griffiths akizungumza katika uzinduzi huo amesema, “ujumbe wangu ni wa dharura: Msiwafungie mlango watu wa Afghanistan. Mashirika ya kibinadamu yako tayari, na yanafanya kazi, licha ya changamoto. Tusaidie kuongeza na kuzuia kuenea kwa njaa, magonjwa, utapiamlo na hatimaye kifo kwa kuunga mkono mipango ya kibinadamu tunayozindua leo.”

Mpango huo uliozinduliwa unahitaji dola bilioni 4.44, ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi cha msaada wa kibinadamu kuwahi kuzinduliwa.

Ikiwa kiwango hicho cha fedha kitapatikana, mashirika ya misaada yanaweza kuimarisha utoaji wa msaada wa kuokoa maisha wa chakula na kilimo, huduma za afya, matibabu ya utapiamlo, makazi ya dharura, upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira, ulinzi na elimu ya dharura.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*