?>

UN: Zaidi ya watu milioni 7 wamekuwa wakimbizi nje ya Ukraine mbali na wakimbizi wa ndani

UN: Zaidi ya watu milioni 7 wamekuwa wakimbizi nje ya Ukraine mbali na wakimbizi wa ndani

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, vita vya Ukraine ni moja ya sababu za ongezeko la wakimbizi ulimwenguni na kwamba hadi hivi sasa mamilioni ya watu wameshakuwa wakimbizi kutokana na vita hivyo.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, umoja huo umesema kuwa, hadi hivi sasa, zaidi ya watu milioni 7 wameshakuwa wakimbizi nje ya Ukraine, na idadi nyingine kubwa mara kadhaa zaidi ya hiyo wamekuwa wakimbizi ndani ya nchi hiyo tangu vilipoanza vita tarehe 24 Februari mwaka huu.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, hivi sasa zaidi ya watu milioni mia moja ni wakimbizi katika kona mbalimbali duniani na kwamba kati ya kila watu 78, mmoja wao anaishi katika mazingira ya ukimbizi ulimwenguni.

Kwa upande wake, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umesema katika ripoti yake kwamba, wakimbizi hao milioni mia moja wanajumuisha watoto wadogo wasiopungua milioni 37. 

UNICEF imesema, mapigano katika nchi za Afghanistan, Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Yemen na maeneo mengine duniani, ndiyo sababu kubwa ya ongezeko hilo lisilo na kiasi la wakimbizi.

Idadi ya watu waliolazimika kukimbia makazi yao ni kubwa katika kona mbalimbali za dunia. Ndio maana Umoja wa Mataifa umeitangaza Juni 20 ambayo mwaka huu imesadifiana na leo Jumatatu, kuwa Siku ya Kimataifa ya Wakimbizi. Fursa ya siku ya leo huwa inatumiwa kimataifa kuenzi na kuwapa heshima watu ambao wamelazimika kukimbia makazi yao na kuishi katika mazingira magumu ya ukimbizi.


342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*