?>

Upeo mpya katika uhusiano wa Iran na Oman kufuatia safari ya Raisi mjini Muscat

Upeo mpya katika uhusiano wa Iran na Oman kufuatia safari ya Raisi mjini Muscat

Kufuatia safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Oman, upeo mpya umefunguliwa katika uhusiano na ushirikiano wa nchi hizi mbili.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni, Barabara na Maendeleo ya Miji, Mafuta, Viwanda na Ulinzi wamefuatana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ziara hiyo inayoashiria kupanuka uhusiano wa nchi hizo katika nyanja tofauti.

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais wa Iran mjini Muscat katika kipindi cha uongozi wa Sultan mpya wa Oman na ya tano ya kigeni ya Rais Raisi katika kipindi cha miezi 9 ya serikali yake ya 13.

Katika safari hii, hati 12 za ushirikiano katika nyanja mbalimbali zimetiwa saini, ambapo jambo hilo linaonyesha hamu ya nchi mbili ya kufikia maendeleo na ustawi wa pande zote katika nyanja mbalimbali.

Kabla ya hapo mawaziri kadhaa na ujumbe wa watu 50 wafanyabiashara na wanauchumi wa Iran walikuwa wamesafiri nchini Oman ili kuandaa uwanja wa kustawishwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi mbili, na hii inaonyesha kuwa uhusiano na ushirikiano wa sekta binafsi za nchi hizo unaenda sambamba na sekta ya umma.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Habari la Oman, makampuni 2,710 ya Iran yamewekeza nchini Oman, ambapo makampuni 1,166 yanamilikiwa na Wairani kwa asilimia 100  na mengine 1,547 yanamilikiwa kwa ushirikiano wa Wairani na Waomani.

Takwimu zilizopo pia zinaonyesha hamu kubwa ya nchi mbili ya kukuza uhusiano wao wa kibiashara na kiuchumi hadi kufikia kiwango cha uhusiano wa kisiasa ambao nchi hizo zimekuwa zikiufurahia katika miaka na miongo iliyopita.

Ingawa kiwango cha mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi kati ya pande mbili kimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, lakini bado kuna njia ndefu kabla ya kufikiwa kiwango kinachohitajika na katika hatua ya kwanza, juhudi zinafanyika ili kuongeza maradufu kiwango cha mabadilishano hayo ya kibiashara na kiuchumi hadi kufikia dola bilioni moja na nusu. Kwa kutilia maanani hali ya sasa, ni rahisi kufikiwa lengo hilo.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba baada ya muda, mwelekeo wa biashara kati ya nchi hizo utapata msukumo mkubwa. Mojawapo ya miundombinu muhimu kwa ajili ya maendeleo na ongezeko la mabadilishano ya biashara ni utengenezaji wa njia za usafiri na mawasiliano kati ya nchi mbili. Kwa maelezo hayo na katika safari hii ya Rais Raisi nchini Oman, pande mbili zimesisitiza udharura wa kuimarishwa usafiri wa baharini kati ya Bandar Abbas nchini Iran na Bandar al-Suwaiq huko Oman, na pia safari za baharini kati ya Chabahar na Muscat. Wakati huo huo njia za kuwezesha usafiri wa baharini na kutatua matatizo katika bandari za Salaha na Swahar nchini Oman kwa ajili ya meli za Iran zimejadiliwa na kuafikiwa.

Katika sekta ya anga, pande mbili zimejadili njia za kuimarisha usafiri wa anga kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman, na pia kuiwezesha Oman ijiunge na makubaliano ya usafiri ya pande tatu ya Chabahar yaliyofikiwa kati ya Iran, India na Afghanistan. Eneo jingine la uhusiano na ushirikiano kati ya Tehran na Muscat ni sekta ya nishati, ambapo makubaliano mapya yamefikiwa wakati wa ziara ya Rais Raisi nchini Oman.

Kuhusiana na hilo, na kwa mwaliko wa Wizara ya Mafuta ya Iran, ujumbe wa ngazi ya juu wa kiufundi kutoka Oman hivi karibuni utasafiri hadi Iran kutembelea vituo vya mafuta na gesi vya Iran na kujifahamisha na uwezo wa wahandisi, wakandarasi na makampuni yanayojihusisha na masuala mbalimbali katika sekta hiyo. Biashara na mauzo ya nje ya bidhaa za petrokemikali pia yalijadiliwa katika mazungumzo ya pande mbili.

Nchi hizo mbili pia zinaweza kuongeza ushirikiano wao katika uga wa utalii kwa sababu kuna fursa nyingi za kutekeleza miradi ya utalii kati ya Muscat na Tehran. Iran na Oman ziko karibu sana kijiografia na zina uhusiano mkubwa wa kihistoria na maslahi ya pamoja.

Kwa hivyo, utalii ni moja ya sekta ambazo zinaweza kunufaika na uwekezaji wa pande mbili. Iran ina maeneo muhimu ya kimaumbile, ya kale na ya kihistoria yenye hali tofuti za hali ya hewa zinazoweza kusaidia kuendeleza ushirikiano wa kitalii. Oman pia ina nyanja nyingi za utalii, ikiwemo milima, maeneo tambarare na majangwa, na  hio linaweza kutumika katika mfumo mzima wa miradi ya utalii.

Kuingia Iran na Oman katika nyuga za kiuchumi na kibiashara kunamaanisha kuwa nchi  mbili hizi zimeamua kutumia uzoefu wao mzuri wa kisiasa, kieneo na kiusalama katika miaka iliyopita, kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kibiashara, na hilo linaonekana wazi katika hamu ya serikali za nchi mbili kwa ajili ya kufanikisha suala hilo haraka iwezekanavyo.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*