?>

Upinzani wa serikali ya Afghanistan dhidi ya mfumo wa uliwali uliopendekezwa na Taliban

Upinzani wa serikali ya Afghanistan dhidi ya mfumo wa uliwali uliopendekezwa na Taliban

Serikali ya Aghanistan kwa kauli moja imezitaka nchi zenye ushawishi katika eneo hili na duniani kuhakikisha kuwa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo haubadilishwi kutoka Jamhuri ya Kiislamu na kuwa wa uliwali na Imarati za Kiislamu.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mohammad Hanif Atmar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan amesema hayo alipozungumza na kundi la watafiti wa nchi hiyo na kutilia mkazo wajibu wa kulindwa na kutiwa nguvu kauli moja ya kieneo na kimataifa ya kuendelea kupambana kwa pamoja na ugaidi na kulindwa mafanikio ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya wananchi wa Afghanistan. Vile vile amesisitizia wajibu wa kuendelezwa juhudi za kupatikana ufumbuzi imara wa kisiasa utakaoimarisha uhuru wa wananchi na kutia nguvu mshikamano wa kitaifa.

Wakati huo huo Amrullah Saleh, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Afghanistan amesema kuwa, mchakato wa mazungumzo na kundi la Taliban ni wa kimaonyesho tu unaolenga kupotosha fikra za walio wengi. 

Sisitizo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan la kupinga kuundwa mfumo wa uliwali na Imarati za Kiislamu nchini humo; pendekezo ambalo kundi la Taliban limesema ndilo lengo lake kuu katika mazungumzo, ni ushahidi wa wazi kwamba, serikali ya Afghanistan haikubaliani kabisa na suala la kuvunjwa katiba ya nchi hiyo.

Kitendo cha kundi la Taliban cha kung'ang'ania kubadilishwa mfumo wa kiutawala wa Afghanistan na kufanywa wa kiliwali na wa Imarati za Kiislamu kinashuhudiwa katika hali ambayo wananchi na serikali ya nchi hiyo mara chungu nzima imetangaza kuwa mazungumzo yoyote ya amani hayapaswi kuifanya muhanga Katiba na demokrasia ya nchi hiyo na kurejea katika mfumo wa kiutawala wa kundi la Taliban.

Hivi karibuni maelfu ya wananchi wa Afghanistan walifanya maandamano katika mji mkuu Kabul wakipiga nara zinazosema "udumu mfumo wa Jamhuri" na "hapana kwa mfumo wa kiliwali." Wananchi hao waliunga mkono kuendelea mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Afghanistan kama ambavyo walitangaza pia uungaji mkono wao kwa vikosi vya usalama na thamani na tunu za Katiba ya nchi hiyo.

Ung'ang'aniaji wa kundi la Taliban wa kuvunjwa mfumo wa hivi sasa wa utawala wa kuanzishwa mfumo wa Imarati za Kiislamu huko Afghanistan umejitokeza katika hali ambayo kama jambo hilo litakubaliwa, basi litavuruga vifungu muhimu sana vya Katiba ikiwemo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambao ndio msingi wa muundo wa nguvu na utawala nchini humo. Mfumo wa hivi sasa unatoa fursa kwa wananchi wa Afghanistan kushiriki katika maamuzi ya nchi yao kupitia chaguzi, lakini mfumo unaopendekezwa na Taliban utawaweka pembeni wananchi na maamuzi yote yatakuwa yanachukuliwa na kundi fulani tu lenye itikadi zake maalumu hata kama itikadi zake hizo na maamuzi yake hayo hayakubaliwi na wananchi.

Hata hivyo kama tulivyosema, katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambao ndio msingi wa Katiba ya Afghanistan, wananchi ndio wenye maamuzi makubwa kuhusu nchi yao, na uchaguzi ndio njia bora ya kuweza kudhihirisha matakwa ya wananchi na kuizuia nchi kuingia katika mfumo wa kidikteta na ukandamizaji.

Wananchi wa Afghanistan bado wanakumbuka machungu ya utawala wa kiimla wa Taliban na madhara yake katika masuala mbalimbali ya nchi hiyo iwe ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi, hivyo hawawezi kabisa kukubali kurejeshwa kwenye mfumo ule ule wa kiutawala wa Taliban. Ni kwa saababu hiyo ndio maana muda wote wananchi wa Afghanistan wanasisitiza kwamba suala la kulindwa msingi mkuu wa Jamhuri ni la lazima katika mazungumzo yoyote yale.

Amma tunapoyatupia jicho matamshi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Afghanistan aliyesema kuwa mchakato wa mazungumzo na kundi la Taliban ni wa kimaonyesho tu unaolenga kupotosha fikra za walio wengi, tutaona kuwa ana haki ya kusema hivyo na sababu yake ni kwamba, kundi la Taliban linaweka vizuizi vingi vinavyokwamisha mazungumzo hayo. Ni wazi kwamba, mazungumzo baina ya Waafghani hayatokuwa na matunda madhali kundi la Taliban linaendelea kung'ang'ania misimamo ambayo yenyewe inajua kuwa itavuruga Katiba na muundo mzima wa kiutawala wa Afghanistan. 

342/
Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

پیام رهبر انقلاب به مسلمانان جهان به مناسبت حج 1441 / 2020
We are All Zakzaky
Hatuukubali muamala wa Karni