?>

Uzushaji tuhuma dhidi ya Iran; kurudiwa kila mara na Marekani siasa za ‘majitaka’ zilizogonga mwamba

Uzushaji tuhuma dhidi ya Iran; kurudiwa kila mara na Marekani siasa za ‘majitaka’ zilizogonga mwamba

Katika kipindi cha siku chache zilizopita tumeshuhudia wimbi jengine jipya la propaganda chafu za Marekani dhidi ya Iran.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kisa na mkasa kilianzia kwenye taarifa iliyotolewa wiki iliyopita na wizara ya sheria ya Marekani iliyodai kuwa Polisi ya Upelelezi ya nchi hiyo FBI imefanikiwa kuzima ile ilichokiita ‘njama’ ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutaka kumteka nyara ‘mwanaharakati mmoja’ ndani ya ardhi ya Marekani.

Katika taarifa hiyo, Audrey Strauss, mwanasheria mkuu wa Marekani wa kitengo cha kusini mwa New York alidai kuwa: serikali ya Iran imeratibu na kufanya ujasusi ndani ya ardhi ya Marekani na kuwaamuru maajenti wake wamteke nyara mtu mmoja mwenye asili ya Iran ndani ya ardhi hiyo na kumrejesha Iran, ili kama watafanikiwa, mtu huyo aonekane ametoweka akiwa hajulikani hatima yake.

Japokuwa tuhuma za aina hii si mpya katika mwenendo wa siasa na sera za kiuadui za Marekani dhidi ya Iran, lakini kwa kuzingatia kwamba zimeibuliwa sambamba na kujiri kadhia kadhaa, kuna kila sababu ya kutaamali na kuzitafakari.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif, siku ya Ijumaa aliandika ujumbe kwenye ukurasa wa twitter kujibu tuhuma hizo na kuihutubu Marekani akisema: Zungumzieni hali yenu wenyewe kabla ya kuwatuhumu wengine.

Zarif aliashiria jinsi maajenti wa Marekani walivyohusika katika mauaji ya rais wa Haiti na walivyofanya jaribio kama hilo dhidi ya rais wa Venezuela na akabainisha kwamba: “watu wenye silaha wenye mfungamano na Marekani wanapanga njama zao ndani ya ardhi ya Marekani kwa ajili ya kuwaua viongozi wa Venezuela na Haiti, huku serikali ya Marekani ikijaribu kwa nguvu zote kuficha uhusiano wake wa kihalifu na watu hao kwa kuwatuhumu wengine kwamba wanatekeleza mpango wa utekaji nyara, jambo ambalo ni la kitoto kabisa na la kuchekesha.”

Hakuna shaka yoyote kuwa historia ya Marekani imejaa vitendo vya mauaji, utekaji nyara watu na kufanya hujuma chungu nzima katika nchi zingine duniani. Ama kuhusiana na propaganda chafu ilizoeneza Washington dhidi ya Iran, tunaweza kuzitathmini kuwa ni mwendelezo wa mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Iran imesimama imara kukabiliana na hulka ya Marekani ya uchu wa kujivutia upande wake katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA; na msimamo huo wa Iran ni jambo zito na lenye gharama kubwa kwa Washington. Ndio maana Marekani inajaribu kutumia mbinu nyinginezo ikiwemo ya kuzusha tuhuma bandia kwa dhana na tamaa kwamba itaweza kuiweka Iran kwenye hali ngumu katika mazungumzo hayo.

Katika mchakato wa mazungumzo hayo ya Vienna, Marekani imeonyesha kuwa imedhamiria kuendeleza hila na mbinu yake ya kuzibana shughuli za nyuklia za Iran kupitia mpango wa kudai kila upande utekeleze kwa wakati mmoja majukumu yake kama yalivyoainishwa katika JCPOA. Lakini wakati huohuo, lengo la kistratejia na kimkakati la Washington ni kupigania na kufanikisha malengo yake ya huko nyuma ya kudai mambo yasiyohusiana na JCPOA na kulinda maslahi yake katika masuala yasiyo ya nyuklia, takwa ambalo kwa mtazamo wa Iran halikubaliki katu.

Tangu miaka kadhaa nyuma, viongozi wa Marekani wamekuwa wakisema, sambamba na mazungumzo, lazima wahakikishe wanaendeleza sera ya mashinikizo dhidi ya Iran na kujipatia fursa zaidi kutoka kwa Tehran.

Kwa maneno mengine inapasa tuseme kuwa, tangu Marekani ilipojitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, tabia yake haijabadilika. Ukweli ni kwamba tangu ilipochukua hatua hiyo, Washington haijarekebisha hata sera yake moja dhidi ya Iran, zaidi ya kuishia kuchukua hatua chache tu zisizo na taathira za maana.

Serikali ya sasa ya Marekani inayoongozwa na Joe Biden, ambayo iliingia madarakani na madai ya kuhakikisha inayafufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kupitia mazungumzo ya Vienna, ingali inaendeleza sera zile zile zilizofeli na kugonga mwamba za serikali iliyopita za mashinikizo ya juu kabisa, ambapo katika mazungumzo ya Vienna ingali imeshikilia misimamo yake isiyo na maana, jambo ambalo linasababisha mchakato wa mazungumzo hayo uchelewe kufikia natija.

Kwa upande mwingine, sinario hii ya kipropaganda ya tuhuma za utekaji nyara imezushwa sambamba na kufanyika kongamano la genge la kigaidi la Munafikina (MKO); na kushiriki maafisa kadhaa wa serikali na maseneta wa Marekani katika kongamano hilo kunaonyesha aina fulani ya mfungamano wenye lengo maalum kati ya harakati hizo za pande kadhaa, ambalo ni kuvunja muqawama na ungangari wa Jamhuri ya Kiislamu…/ 

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*