?>

Vipengele vya "Hati ya Heshima ya Palestina" kwa ajili ya kukabiliana na mapatano ya kuanzisha uhusiano rasmi na Israel

Vipengele vya

Makundi ya Kipalestina, jana Jumapili Februari 21 yalikutana Ukanda wa Gaza na kusaini "Hati ya Heshima ya Palestina" katika kuonyesha upinzani wao dhidi ya uanzishaji uhusiano wa kawaida wa vyombo vya habari na utawala haramu wa Kizayuni.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Katika kipindi cha nusu ya pili ya mwaka uliopita wa 2020, baadhi ya nchi za Kiarabu zilichukua hatua ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Nchi nne za Imarati, Bahrain, Morocco na Sudan zilitangaza uamuzi huo hadharani; na baadhi ya nchi zilipanua na kustawisha uhusiano wao na Israel bila ya kubainisha hadharani jambo hilo.

Uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ulikabiliwa na upinzani wa makundi ya Palestina. Aghalabu ya upinzani ulioonyeshwa dhidi ya uamuzi huo ulikuwa wa kisiasa wa kutoa kauli tu za kukemea na kulaani. Jitihada kadhaa pia zilifanywa kwa madhumuni ya kumaliza tofauti baina ya makundi ya Kipalestina ili kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya Serikali ya Mamlaka ya Ndani Ya Palestina kutangaza kuwa, iko tayari kufufua mazungumzo na mashirikiano ya kiusalama na utawala haramu wa Israel.

Kwa sasa tunaweza kusema, kusainiwa Hati ya Heshima ni hatua muhimu iliyochukuliwa na makundi ya Palestina kwa ajili ya kukabiliana na mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel. Hati hiyo imejikita kwenye "vyombo vya habari" na ina vipengele kadhaa muhimu, ambavyo ni:

Mosi, shakhsia wa Palestina kuvisusia vyombo vya habari vya Israel na vya nchi zilizofanya mapatano na utawala huo haramu. Kwa mujibu wa hati hiyo, makundi na mirengo ya kitaifa na Kiislamu ya Palestina imesisitiza kuhusu ulazima wa kukabiliana na uanzishaji uhusiano wa kawaida wa "vyombo vya habari" na utawala ghasibu wa Kizayuni; na imetangaza kuwa, si tu haitafanya mahojiano na chombo chochote cha habari cha Kizayuni, lakini pia haitakuwa tayari kushiriki kwa namna yoyote ile katika vipindi vya kanali za habari ambazo zinawashirikisha shakhsia wa Kizayuni katika vipindi vyao. Kwa maneno mengine ni kwamba, ikiwa chombo cha habari cha nchi ya Kiarabu kitawakaribisha shakhsia kutoka Israel, shakhsia wa Kipalestina watahakikisha hawafanyi mahojaino na mazungumzo na chombo hicho; na yeyote atakayekiuka makubaliano hayo atakuwa amefanya kosa.

Pili, wanaharakati wa vyombyo vya habari vya utangazaji na magazeti vya Palestina wameahidi kwamba hawatashiriki katika mkutano, kongamano au warsha yoyote ambayo itaendeshwa na mwakilishi rasmi au asiye rasmi wa Kizayuni.

Tatu, ni kuanzisha mahubiri ya vyombo vya habari ya kitaifa ya Palestina. Mbali na mahubiri na mazungumzo hayo kujumuisha ufuataji sera ya pamoja ya vyombo vya habari ya kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida, yataitangaza pia Palestina kuwa ndilo lengo kuu na la kwanza la umma wa Kiarabu na Kiislamu. Kuhusiana na nukta hiyo, Khalid al Batsh, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Jihadul Islami ya Palestina, ambaye alihudhuria hafla ya utiaji saini Hati ya Heshima ya Palestina hapo jana, alitilia mkazo umuhimu wa kupitishwa hati ya pamoja ya kitaifa ya mahubiri ya vyombo vya habari kwa ajili ya kukabiliana na kila aina ya uanzishaji uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni; na akasema, Palestina inapasa ibaki kuwa lengo tukufu la kwanza la umma wa Kiarabu na Kiislamu.

Kipengele cha nne kinahusu lengo linalofuatiliwa na Hati ya Heshima. Lengo kuu la maamuzi yaliyopitishwa kwenye hati hiyo na sera ya pamoja ya vyombo vya habari ni kuzuia ushawishi na satua ya Wazayuni ndani ya umma wa Kiislamu kupitia kushirikishwa kwao mara kwa mara katika vyombo vya habari vya Kiarabu na Kiislamu na kupitia uanzishaji wa uhusiano wa kawaida wa vyombo vya habari. Lengo jengine linalofuatiliwa na Hati ya Heshima ni kuhakikisha kwamba, badala ya kungojea msaada na uungaji mkono wa nje, makundi ya Kipalestina yalinde na kudumisha nafasi na hadhi ya kadhia na lengo tukufu la Palestina katika nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Kuhusiana na jambo hilo, Hani Ath-Thawaabitah, mjumbe wa kamati kuu ya harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Palestina amesema: "Hatua za mtawalia zinazochukuliwa kwa madhumuni ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Kizayuni katika eneo la nchi za Kiarabu, zinaonyesha udharura uliopo wa kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na aina zote za uanzishaji uhusiano wa kawaida, ukiwemo wa vyombo vya habari. Sauti zinazosikika katika eneo, za kuanzisha uhusiano wa kawaida wa vyombo vya habari zinapazwa kwa nia ya kudhoofisha hisia za uelewa za mataifa, kuipamba sura chafu ya utawala ghasibu wa Kizayuni na kushiriki katika kuiporomosha nafasi na hadhi ya lengo tukufu la ukombozi wa Palestina katika nchi za Kiarabu na Kiislamu."

Nukta ya kumalizia ni kwamba, Hati ya Heshima ya Palestina inamaanisha imani ya makundi ya Kipalestina ya "kujitegemea" katika kuilinda Palestina na kukabiliana na uanzishaji wa uhusiano kupitia sera ya pamoja ya vyombo vya habari; lakini umuhimu wa hati hiyo utaongezeka pale makundi hayo pamoja na shakhsia wa Kipalestina watakapoivuka awamu ya kinadharia na kuingia kwenye hatua ya utekelezaji kivitendo wa hati hiyo.../

342/
Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*

پیام رهبر انقلاب به مسلمانان جهان به مناسبت حج 1441 / 2020
We are All Zakzaky
Hatuukubali muamala wa Karni