?>

Wafanyakazi wa Yemen; wahanga wakuu wa hujuma ya muungano wa Saudia

Wafanyakazi wa Yemen; wahanga wakuu wa hujuma ya muungano wa Saudia

Licha ya kuwa vita vya muungano wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimekuwa na wahanga wengi lakini takwimu zinaonyesha kwamba wafanyakazi ndio wahanga wakuu wa vita hivyo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Miezi 74 imepita tangu kuanzishwa vita hivyo visivyo na uwiano dhidi Yemen.  Vita hivyo vilianzishwa katika hali ambayo nchi hiyo ilikuwa na ingali ni nchi masikini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu.Vita dhidi ya Yemen vimekuwa na maadhara makubwa kwa watu wa nchi hiyo na hasa tabaka la watu masikini na wale wanaofanya kazi za sulubu.

Kwa mnasaba wa Siku ya Wafanyakazi Duniani au kwa jina jingine Leba Dei, chama cha wafanyakazi wa Yemen, kimetoa ripoti kikisema kwamba moja ya taathira za wazi na za moja kwa moja za vita vya Muungano wa Saudia dhidi ya taifa la Yemen ni kuuawa wafanyakazi 10,900 na kujeruhiwa wengine 19,500. Kwa takwimu hizo tunaweza kusema kuwa nusu ya watu waliouawa kwenye vita hivyo ni wafanyakaza wa kazi za mikono na za sulubu.

Nukta nyingine muhimu ni kwamba kifo hakihesabiki kuwa ni mwisho wa maisha tu bali ni mwanzo wa masaibu na matatizo kwa wafiwa na familia zinazoachwa nyuma. Kuuawa kwa wafanyakazi wapatao elfu 11 wa Yemen kuna maana ya mamia ya familia kupoteza watu wanaozidhaminia mkate na mahitaji ya kila siku. Kwa mameno mengine ni kwamba kuuawa watu wanaodhamini na kukidhi mahitaji ya familia huwa na taathira kubwa na ya moja kwa moja kwa wafiwa na hivyo kuongeza matatizo ya kijamii kwenye familia na vile vile katika upeo wa kitaifa.

Suala jingine ni kwamba wafanyakazi wa kazi za mikono wa Yemen wamepoteza vyanzo vya mapato yao. Kutokana na vita vya Muungano wa Saudia, asilimia 80 ya miundomsingi ya Yemen vikiwemo viwanda, maduka, masoko, hospitali, viwanja vya ndege na barabara imeharibiwa kabisa. Wakati huo huo shughuli za kawaida katika miradi ya maendeleo zimesimama kutokana na milipuko ya mara kwa mara ya mabomu yanayodondoshwa kila siku na maadui kwenye vichwa vya watu wa nchi hiyo.

Kwa msingi huo ripoti ya chama cha wafanyakazi wa Yemen imesema kwamba mashambulio ya muungano huo na mzingiro uliowekwa dhidi ya Yemen vimeongeza uhaba wa ajira katika nchi hiyo hadi kufikia asilimia 65 na kiwango cha umasikini kufikia asilimia 80. Ni wazi kuwa mashambulio ya Saudia dhidi ya Yemen yameibua maafa na hali ya kutisha kwa watu wa nchi hiyo. Ni kutokana na ukweli huo ndio maana Umoja wa Mataifa ukatangaza mara kadhaa kwamba Yemen inakabiliwa na maafa makubwa zaidi ya kibinadamu kuwahi kushuhudiwa duniani katika karne ya 21.

Kufikia sasa Umoja wa Mataifa na taasisi zilizo chini yake zimetangaza kwamba raia wa Yemen karibu milioni 21 wanakabiliwa na tatizo kubwa la kutokuwa na usalama wa chakula, lugha inayotumiwa na umoja huo kumaanisha kuwa watu hao wanakabiliwa na baa la njaa.

Mark Lowcock, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura ya Umoja huo alisema katika ripoti aliyotoa Februrai mwaka huu kwamba karibu asilimia 80 ya watu wa Yemen wanahitajia misaada ya chakula na kwamba watoto laki nne wa nchi hiyo wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na tatizo la utapiamlo. Aliongeza kwamba: Licha ya kwamba hata kabla ya vita, Yemen ilikuwa nchi masikini iliyokabiliwa na tatizo la utapiamlo na njaa, lakini uchumi wake ulikuwa ukifanya kazi ambapo serikali ilikuwa ikitoa huduma za dharura kwa idadi kubwa ya raia wake. Lakini kwa sasa vita vimeharibu kila kitu. Mgogoro wa chakula umepelekea nchi hiyo kukumbwa na baa kubwa zaidi la njaa kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya karibuni duniani.

Hata kama matabaka yote ya watu wa Yemen yanakabiliwa na hali hiyo ya kusikitisha lakini ni wazi kuwa tabaka la wanaofanya kazi za sulubu na familia zao ndio wameathirika zaidi na vita hivyo na hivyo kuwa wahanga wakuu wa vita vya kichokozi vya Muungano wa Saudia dhidi ya Yemen.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*