?>

Yamkini Saudia ikaongeza idadi ya Wairani wanaoenda Hija mwaka huu

Yamkini Saudia ikaongeza idadi ya Wairani wanaoenda Hija mwaka huu

Waziri wa Hija na Umrah wa Ufalme wa Saudi Arabia amesema wizara hiyo inatafakari kuongeza idadi ya raia wa Iran watakaoenda Hija mwaka huu.

Ripoti ya shirika la habari la Ahlul Bayt(as)- ABNA - Tawfiq Al Rabiah ametoa tamko hilo katika mkutano na Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara za Kidini Iran Sayyid Sadiq Husseini katika kikao kilichofanyika Jeddah.

Mwaka huu wakuu wa Saudia wameidhinisha Wairani 39,635 kutekeleza ibada ya Hija. Hata hivyo kutokana na kuwa idadi kubwa ya Wairani wako katika zamu wakisubiri fursa ya kutekeleza ibada ya Hija, maafisa wa Iran wamewasilisha ombi kwa Saudia kuongeza idadi hiyo mwaka huu.

Al Rabiah amesema kwa kuzingatia kuwa Waislamu kutoka nchi kadhaa wameakhirisha safari za Hija mwaka huu kutokana na sababu mbali mbali, kunafanyika tathmini ya kuongeza idadi ya Wairani watakoenda Hija mwaka huu.

Kwa upande wake, Husseini ameelezea matumaini yake kuwa diplomasia ya Hija baina ya Iran na Saudia itapelekea kutatuliwa hitilafu za kisiasa baina ya pande mbili. Aidha amesema anatumai kuwa, kwa msaada wa Saudia, Wairani wataanza tena kutekeleza ibada ya Hija ndogo au Umrah. Husseini aidha amesema kwa sasa Wairani zaidi ya milioni 1.2 wamejiandikisha kutekeleza ibada ya Hija na hivyo ameitaka Saudia kufanya mpango ili watimize wajibu wao wa kidini.

Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara za Kidini Iran pia amelalamika kuhusu ongezeko kubwa la gharama ya Hija mwaka huu na hivyo ametoa wito kwa wakuu wa Saudia kuchukua hatua za kupunguza mzigo wa kifedha wa Mahujaji kutoka maeneo yote ya dunia.

Waziri wa Hija wa Saudia amesema gharama za Hija zimepanda kutokana na ongezeko jumla la gharama za maisha duniani na kuongeza kuwa serikali ya Saudia imejitahidi kutoa huduma kwa gharama za chini kabisa ili kuwasaidia Mahujaji.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*