?>

Zaidi ya watu milioni 15 wameambukizwa corona duniani katika kipindi cha wiki moja

Zaidi ya watu milioni 15 wameambukizwa corona duniani katika kipindi cha wiki moja

Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa, zaidi ya watu milioni 15 wamekumbwa na ugonjwa wa UVIKO-19 yaani corona duniani katika kipindi cha wiki moja.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom ametoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari na kuonya kwamba idadi hiyo inaweza kuwa si halisi, bali idadi ya wagonjwa wa corona katika kipindi cha wiki moja duniani ni zaidi ya watu milioni 15.

Amesema, idadi hii kubwa ya maambukizi ya corona duniani inatokana na kuenea kwa kasi kirusi cha Omicron ambacho uambukizaji wake unaendelea kuupiku kwa kasi kubwa ule wa kirusi cha Delta katika takriban nchi zote duniani.

Hata hivyo ametoa taarifa ya kutia moyo inayosema kuwa, idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa UVIKO-19 haijapanda tangu mwezi Oktoba 2021 na kwamba wastani wa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa corona ni watu 48,000 kwa wiki. Pamoja na hayo amesema, idadi hiyo ya vifo bado ni kubwa sana.

Katika taarifa yake hiyo, Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO amesema, ni vyema tuseme wazi kwamba, ijapokuwa kasi ya maambukizo ya kirusi cha Omicron ni kubwa, lakini idadi yake ya vifo vyake ni ndogo ikilinganishwa na Delta. Pamoja na hayo kirusi hicho kipya bado ni tishio na ni hatari hasa kwa watu ambao hawajapiga chanjo.

Ameyataka mataifa ya dunia yasilegeze kamba katika kupambana na corona kama ambavyo pia amewataka watu duniani wajitokeze kupiga chanjo kamili ili kujilinda na ugonjwa huo.

342/


Tuma maoni

Email yako haiwezi kutuma, tafadhali chunguza Email yako

*